Hakika hapana shaka yoyote kwamba kumpenda Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni jambo linalopaswa kuwepo ndani ya moyo wa kila muislamu, juu zaidi kuliko mapenzi yake kwa baba yake, mama yake, mwanawe wa kiume na wa kike, kwa sababu ya maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hatoamini mmoja wenu mpaka niwe ninayependwa zaidi kwake kuliko baba yake, mwanawe, na watu wote.”

Ameipokea al-Bukhaariy (15) na Muslim (169) kupitia kwa Anas (Radhiya Allaahu ´anh).

Alama iliyo wazi na bayana kabisa ya kumpenda Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kumuiga na kufuata njia yake, kama alivyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):

قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّـهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّـهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ

“Sema: “Mkiwa mnampenda Allaah, basi nifuateni mimi. Hivyo atakupendeni Allaah na atakusameheni dhambi zenu na Allaah ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.”[1]

Hii ndiyo kipimo halisi cha mapenzi ya kweli kwa Mtume – si madai tu ya mdomoni bali ni utekelezaji kwa kufuata Sunnah zake na kuishi kwa mujibu wa muongozo wake.

[1] 03:31

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-Muhsin bin Hamad al-´Abbaad
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 86-87
  • Imechapishwa: 05/07/2026