59. Ni wajibu kuwa na subira juu ya misiba

Allaah (Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اصْبِرُوا وَصَابِرُوا وَرَابِطُوا وَاتَّقُوا اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ

“Enyi mlioamini! Subirini na zidisheni kuvuta subira na kuweni [daima] macho [kupambana kwa ajili ya imani] na mcheni Allaah ili mpate kufaulu.” 03:200

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَعِينُوا بِالصَّبْرِ وَالصَّلَاةِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ مَعَ الصَّابِرِينَ

”Enyi mlioamini! Tafuteni msaada kwa subira na swalah! Hakika Allaah yuko pamoja na wanaosubiri.” 02:153

وَلَنَبْلُوَنَّكُمْ حَتَّىٰ نَعْلَمَ الْمُجَاهِدِينَ مِنكُمْ وَالصَّابِرِينَ وَنَبْلُوَ أَخْبَارَكُمْ

”Bila ya shaka Tutakujaribuni mpaka tutambue wenye wale wenye kupambana na kufanya bidii miongoni mwenu na wenye kuvuta subira na Tutazijaribu habari zenu [kuona ukweli wake zilivyo].” 47:31

Aayah zinazozungumzia subira ni nyingi sana. Imam Ahmad amesema:

“Allaah ametaja katika Qur-aan subira mara 90.”

Kwa mujibu wa viongozi wa Taswawwuf subira ni sifa nzuri inayoizuia nafsi kufanya yote ambayo ni mabaya na ni nguvu inayoifanya nafsi kuwa imara. Sa´iyd bin Jubayr amesema:

“Subira ni mja kujitambulisha mbele ya Allaah ya kwamba msiba wake unatoka Kwake na kwamba anatarajia kupata thawabu Zake.”

Usaamah bin Zayd amesema:

“Tulikuwa pamoja na Mtume (Swalla Allaahu alayhi wa sallam) pindi mmoja katika wasichana zake alipomtumia mjumbe kumweleza kuwa mtoto wake amefariki. Akamwambia yule mjumbe: “Rudi umwambie kuwa ni cha Allaah kile Alichokitoa na kukichukua na kila kitu Kwake kina muda maalum. Mwamrishe awe na subira na atarajie malipo kutoka kwa Allaah.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Alimwamrisha kusubiri.

Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipita karibu na mwanamke anayelia kwenye kaburi. Akamwambia: “Mche Allaah na uwe na subira.” Mwanamke yule akasema: “Toka karibu yangu. Hukufikwa na msiba uliyonifika.” Hakumjua. Alipokuja kujua kuwa ni Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaenda kwenye mlango wake na hakukuta walinzi wa mlango. Akamwambia: “Sikukujua.” Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia: “Hakika subira inakuwa katika kile kipindi cha kwanza msiba unakugonga.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim. Katika upokezi mwingine imetajwa ya kwamba alikuwa anamlilia mtoto wake wa kiume aliyekufa. Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Hakika subira inakuwa katika kile kipindi cha kwanza msiba unakugonga.”

Haya yanashabihiana na maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mwenye nguvu sio yule mwenye kushinda wakati wa miereka. Mwenye nguvu ni yule anayeimiliki nafsi yake wakati wa hasira.”

Kusononeka wakati wa msiba kunaufanya moyo kuingiwa na khofu ambako kunamuudhi yule mtu pindi anapofikiwa na khabari hizo. Mtu akisubiri kile kipindi cha kwanza umemgonga, hauwi na nguvu kukabiliana nao. Hapa inakuwa ni rahisi kustahamili huko mbeleni. Hali kadhalika hasira.

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah (´Azza wa Jall) anasema: “Nikichukua roho ya kipenzi wa mja wangu muumini kutoka katika dunia hii kisha akatarajia malipo kutoka kwa Allaah sina jengine cha kumlipa isipokuwa Pepo.”

Ameipokea al-Bukhaariy.

´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia ya kwamba alimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu tauni. Akamwambia:

“Ni adhabu ambayo Allaah anaituma kwa anayemtaka. Anaifanya kuwa ni rehema kwa waumini. Kukitokea tauni na mja akabaki katika mji wake akisubiri na kutarajia malipo kutoka kwa Allaah na akatambua kuwa hakuna kitachomfika isipokuwa kile ambacho Allaah amemuandikia, isipokuwa atakuwa na ujira kama wa shahidi.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Imaam Ahmad.

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

“Wanachuoni wameafikiana kuwa ni wajibu kusubiri wakati wa misiba. Walichotofautiana ni kama ni wajibu kuridhia.”

Ni wajibu kuwa na subira kwa jumla. Hata hivyo imekokotezwa kutegemea na wakati. Imekokotezwa zaidi kuwa na subira kipindi cha tauni kuliko nyakati zingine. Ikiwa mtu anaishi katika mji ambapo tauni imezuka, akasubiri kwa kufa watoto, jamaa na marafiki zake na akasubiri kwa msiba wake yeye mwenyewe na akawa na yakini kuwa mauti hayatosogea mbele wala hayatorudi nyuma na kwamba Allaah ameandika muda wa kuishi pindi vipomoko vilipokuwa tumboni mwa mama zao na akatarajia malipo kutoka kwa Allaah, atalipwa Pepo. Hata hivyo ikiwa mtu atakata tamaa na asisubiri, atakuwa amefanya dhambi na kujichosha mwenyewe na hatobadilisha kitu kutoka katika yale Allaah aliyopanga.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 132-134
  • Imechapishwa: 29/10/2016