59. Ni lini inawajibika Zakaah? Ni wepi wenye kuiistahiki?

Swali: Ni lini inawajibika Zakaah? Ni wepi wenye kuiistahiki?

Jibu: Zakaah inawajibika kwa muislamu ambaye ni muungwana na anamiliki kiwango cha wajibu kilichopitikiwa mwaka mzima, hapo atalazimika kukitolea zakaah. Kiwango cha wajibu cha dhahabu ni gramu 92 na fedha ni gramu 595. Pindi mmiliki anapomiliki kiwango hicho mwaka mzima, basi anatakiwa kukitolea zakaah 2,5%. Ni takriban SAR 2.5 kwa SAR 100, SAR 25 kwa SAR 1000.

Wakati wa kuwajibika kwake ni kuanzia pale ambapo mtu anamiliki kiwango hicho kikapitikiwa na mwaka mzima. Kama umemiliki kiwango hicho Muharram, basi unawajibika kutoa zakaah Muharram mwaka unaofuata na kadhalika. Ulazima wa zakaah haikufungamana na Ramadhaan. Waislamu wanahakikisha kuzitolea zakaah mali zao katika Ramadhaan kutokana na kule thawabu kulipwa maradufu mwezi huo. Yule ambaye mali yake imekamilisha mwaka mzima katika mwezi usiokuwa Ramadhaan, basi analazimika kuitoa kipindi hicho na wala asiicheleweshi mpaka Ramadhaan. Lakini hata hivyo haina neno akiiharakisha kuitoa kabla ya kupitikiwa na mwaka katika Ramadhaan.

Kuhusu wale watu wanaoistahiki, Allaah (Ta´ala) anasema:

إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاءِ وَالْمَسَاكِينِ وَالْعَامِلِينَ عَلَيْهَا وَالْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ وَفِي الرِّقَابِ وَالْغَارِمِينَ وَفِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَابْنِ السَّبِيلِ ۖ فَرِيضَةً مِّنَ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ

“Hakika si venginevyo zakaah ni kwa ajili ya mafakiri na masikini na wanaozitumikia na wanaotiwa nguvu nyoyo zao [kwa ajili ya Uislamu] na kuwakomboa mateka na wenye deni na katika njia ya Allaah na msafiri [aliyeharibikiwa] – ni faradhi itokayo kwa Allaah; na Allaah ni Mjuzi, Mwenye hekima.”[1]

[1] 9:60

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah Aalush-Shaykh
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Min Fataawaas-Swiyaam, uk. 46
  • Imechapishwa: 08/04/2022