58. Salaf walivyokuwa wakikabiliana na msiba

Nimeona kwenye kitabu, ambacho sumjui mwandishi wake na kisichokuwa na mwanzo, namna Zayd bin Aslam alivyosema:

“Mtoto wa Daawuud (´alayhis-Salaam) alifariki. Akasononeka na watu wakaja kumpa pole. Akaambiwa: “Alikuwa na uzito gani?” Akasema: “Nilikuwa nampenda zaidi ya dunia nzima iliyojaa dhahabu.” Kukasemwa: “Unapata thawabu mfano wa hivo.”

Katika mapokezi ya kiisraeli kuna ya kwamba mtoto wa Sulaymaan (´alayhis-Salaam) alikufa. Akasononeka mapaka ikajulikana. Wakaja Malaika wawili katika umbile la wanaadamu kumuomba awahukumu. Mmoja wao akasema: “Huyu amepanda kwenye njia ambayo watu wanapita. Nikapita na nikawa nimeiharibu.” Sulaymaan akasema kumwambia yule mwingine: “Kwa nini umepanda njiani? Hukujua kuwa watu wanapita hapo?” Yule mtu akasema: “Kwa nini na wewe unasononeka juu ya mwanao? Hujui kuwa hii ni njia ya watu kuelekea Aakhirah?”

Usaamah bin Zayd amesema:

“Tulikuwa pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pindi mmoja katika wasichana wake alipomtuma mjumbe kumweleza kuwa mtoto wake amekufa. Akamwambia mjumbe yule: “Rudi umwambie kuwa ni cha Allaah kile Alichokitoa na kukichukua na kila kitu Kwake kina muda maalum. Mwamrishe awe na subira na atarajie malipo kutoka kwa Allaah.” Baada ya hapo yule mjumbe akarudi na kusema: “Ninaapa unatakiwa uje kwake.” Mtume (Swalla Allaahu alayhi wa sallam) akasimama akiwa pamoja na Sa´d bin ´Ubaadah, Mu´aadh bin Jabal, ´Ubayy bin Ka´b, Zayd bin Thaabit pamoja na mimi. Mtoto mdogo akaja anamkimbilia na moyo wake unagonga utafikiri ni chupa dogo. Machozi yakamlenga. Sa d akamwambia: “Ee Mtume wa Allaah! Ni nini?” Akasema: “Ni huruma ambao Allaah ameuweka kwenye mioyo ya waja. Allaah anawahurumia katika waja Wake wale wenye kuhurumia.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

al-Hasan al-Baswriy amesema:

“Hakuna hasira inayopendwa na Allaah sana kama msiba wenye kuumiza unaokabiliwa kwa faraja na subira na ghadhabu inayokabiliwa kwa upole.”

Imepokelewa ya kwamba Shimr alikuwa akisema kumwambia aliyepatwa na msiba:

“Kuwa na uvumilivu juu ya hukumu ya Mola wako.”

Ibn Abiy Dunyaa amepokea kutoka kwa ´Abdullaah bin Muhammad bin Ismaa´iyl at-Taymiy ya kwamba kuna ambaye alimpa pole mtu kwa sababu ya mwanaye na kusema:

“Allaah huitimiza ahadi Yake kwa yule mwenye kuvumilia kwa sababu Yake. Kwa hiyo kuwa mwangalivu usikusanye msiba wako na thawabu za kusibiwa na msiba. Huu ni msiba mkubwa kwako.”

Ibn-un-Simaak alimpa mtu pole na kumwambia:

“Ni juu yako kuwa na subira. Hivyo ndivyo anavyokuwa yule anayetaka kupewa thawabu na huko ndiko anakoenda yule mwenye kusononeka.”

´Ubayd bin ´Umayr amesema:

“Kukata tamaa sio kutokwa na machozi na moyo kuingiwa na huzuni. Kukata tamaa ni maneno na dhana mbaya.”

Khaalid bin Abiy ´Uthmaan al-Qurashiy amesema:

“Sa´iyd bin Jubayr alinipa pole pindi baba yangu alipofariki. Katika mnasaba fulani akaniona natufu Ka´bah hali ya kuwa niko na maski. Akanivua nayo kichwani na kusema: “Kujificha ni kukata tamaa.”

al-Bayhaqiy amepokea kwa mlolongo wa wapokezi wake katika “Manaaqib-ush-Shaafi´iy” ya kwamba mtoto wa ´Abdur-Rahmaan bin Mahdiy alifariki na akawa amehuzunika kiasi kikubwa. ash-Shaafi´iy (Rahimahu Allaah) akamwandikia akimwambia:

“Ndugu mpendwa! Jiliwaze kwa yale unayowaliwaza wengine. Yadharau matendo yako kama jinsi unavyoyadharau ya wengine. Tambua kuwa msiba mkubwa ni kukosa furaha na thawabu yote mawili. Mtu asemeje ikiwa utaongezea juu yake kufanya dhambi?”

Swaalih al-Murriy alimwambia mtu ambaye amefiliwa na mwanaye:

“Ikiwa msiba wako umekufanya kupata mafunzo basi msiba wako ni msiba bora kabisa. Ikiwa msiba wako haukukupa mafunzo yoyote basi msiba wako ni mkubwa kuliko msiba wa mwanao.”

Kuna mtu alimpa pole mwengine. Yule mtu akasema:

“Ndugu yangu! Mwenye busara hufanya ile siku ya kwanza yanayofanywa na mjinga baada ya mwaka mmoja.”

Kuna mtu alimpa pole mwengine. Yule mtu akasema:

“Yule ambaye anakupa ujira Aakhirah ni bora kuliko yule anayekupa furaha hapa duniani.”

“Yule asiyekabiliana na msiba wake kwa kuwa na subira na kutarajia malipo kutoka kwa Allaah huukandamiza kama mnyama.”

Baadhi ya Salaf wamesema:

“Ukisubiri utakuwa na msiba mmoja. Usiposubiri utakuwa na misiba miwili.”

Maymuun bin Mahraan ameeleza ya kwamba kuna mtu alimpa pole ´Umar bin ´Abdil-´Aziyz kwa sababu ya mtoto wake ´Abdul-Malik. Ndipo ´Umar akasema:

“Yaliyomfika ´Abdul-Malik ni kitu tulichokuwa tunajua kuwa kitapitika. Kilipotokea haikuwa ni kitu kipya kwetu.”

Ibn ´Asaakiyr amepokea namna ambavyo ash-Shaafi´iy alimtumia pole mmoja katika marafiki zake kutoka katika Quraysh ambaye alikuwa amefiliwa na mwanaye. Akaandika:

“Ndugu mpendwa! Tambua kuwa kila msiba usiomfanya mwenye nao kupata thawabu basi ni msiba mkubwa. Ndugu mpendwa! Ni vipi utaridhia pindi mtoto wako anapopewa mtihani na huridhii pindi anaponeemeshwa? Ni vipi utaridhia anapotiwa katika ufisadi na huridhii pindi anapokuwa na sifa njema? Vipi utamchukia yule mwenye kukuneemesha ikiwa hutambua neema Zake? Anakuonyesha kile anachokipenda na anakuficha kile anachokichukia. Rejea kwa Allaah (´Azza wa Jall), jiliwaze kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na shikamana na dini yako.

Mtoto wa Ibn ´Asaakir alikufa kabla ya kubaleghe. Akasema:

“Namshukuru Allaah. Sikudhihirisha kukata tamaa wala kuchukia wakati alipokufa. Huzuni haukunifanya kuacha masomo. Nilikuwa bado niko katika hali nzuri na kuongea na watu. Hayo hayakuwa isipokuwa kwa uafikishwaji na msaada wa Allaah. Aliniepusha na kukata tamaa. Shukurani zote ni za Allaah ambaye hakubatilisha thawabu zangu kwake na wala hakuondosha subira yangu niliposhtuka. Mwenye kunyimwa ni yule anayekosa thawabu zake nyingi. Mwenye kulaumiwa ni yule mwenye kukata tamaa kwa sababu ya maumivu ya msiba. Mmoja katika ndugu zangu alishangaa juu ya subira yangu pindi alipokuja kunipa pole na kuninasihi kuvumilia. Akanambia: “Siku ya pili ya msiba nilikupitia pindi ulipokuwa umesimama na kufunza kundi la watu. Nilishangazwa na nguvu zako za kufunza katika kipindi kile.” Nikamwambia kuwa kukata tamaa hakurudishi kile kilichotoweka na kulia hakumsaidii kitu muislamu. Mambo yakishakuwa namna hiyo ni bora zaidi kwa wale warevu na watu wa dini kustahamili.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 124-131
  • Imechapishwa: 28/10/2016