58. Radd juu ya utata wa tatu: kuwaomba uombezi maiti sio shirki

Akisema: “Je, wewe unapinga uombezi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kuikana?” Mwambie: “Siipingi na wala siikani, bali yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye muombezi wa waombezi na nataraji kupata uombezi wake, lakini maombezi yote ni ya Allaah (Ta´ala). Kama alivyosema (Ta´ala):

قُل لِّلَّـهِ الشَّفَاعَةُ جَمِيعًا

”Sema: “Uombezi wote ni wa Allaah.”” (az-Zumar 39 : 44)

Na wala hautofanya kazi isipokuwa baada ya idhini ya Allaah. Kama alivyosema (Ta´ala):

مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِندَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ

”Nani huyu ambaye anashufai mbele Yake bila ya idhini Yake?” (al-Baqarah 02 : 255)

Na wala Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hatomwombea yeyote isipokuwa baada ya Allaah kumruhusu. Kama alivyosema (Ta´ala):

وَلَا يَشْفَعُونَ إِلَّا لِمَنِ ارْتَضَىٰ

”Na wala hawamuombei yeyote isipokuwa kwa yule ambaye Amemridhia.” (al-Anbiyaa´ 21 : 28)

Na Yeye (Subhaanah) haridhii jengine isipokuwa Tawhiyd. Kama alivyosema (Ta´ala):

وَمَن يَبْتَغِ غَيْرَ الْإِسْلَامِ دِينًا فَلَن يُقْبَلَ مِنْهُ

”Na yeyote anayetaka dini isiyokuwa ya Kiislamu basi haitokubaliwa kwake.” (Aal ´Imraan 03 : 85)

Ikiwa uombezi wote ni wa Allaah na wala hautokuwa isipokuwa baada ya idhini Yake, na wala Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala mwengine hawatomwombea yeyote mpaka Allaah amruhusu – na wala Allaah haridhii isipokuwa watu wa Tawhiyd – imekubainikia ya kwamba uombezi wote ni wa Allaah. Hivyo basi, mimi nautafuta kutoka Kwake. Ninasema: “Ee Allaah, usiniharamishie uombezi wake, Ee Allaah, ninakuomba aniombee” na mfano wa haya.

MAELEZO

Uombezi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuna anayeupinga isipokuwa mapote potevu kama vile Khawaarij na Mu´tazilah. Kuhusu Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah miongoni mwa misingi ya ´Aqiydah yao ni kukubali uombezi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), mawalii na waja wema. Lakini hata hivyo hauombwi kutoka kwao ilihali wameshakufa. Unaombwa kutoka kwa Allaah kwa kuwa hakuna yeyote atayeombea mbele ya Allaah isipokuwa baada ya idhini Yake. Ni lazima vilevile yule mwenye kuombewa awe ni miongoni mwa wale wanaoridhiwa na Allaah. Kwa msemo mwingine awe miongoni mwa watu wa Tawhiyd. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye ndiye muombezi mkubwa siku ya Qiyaamah, waliosimama uwanjani watapomsogelea na kumuomba awaombee kwa Allaah awahukumu waja, hatoombea moja kwa moja. Bali atamuomba idhini Mola wake na kumuomba amuidhinishe uombezi ambapo atasujudu mbele Yake, amuombe na kunyenyekea Kwake. Ataendelea katika hali hiyo mpaka Aambiwe:

“Ee Muhammad, inua kichwa chako, omba utapewa na ombea utasikizwa!”[1]

Ni vipi unatakiwa kuomba uombezi? Uombezi unatakiwa kuuomba kutoka kwa Allaah na sio kutoka kwa viumbe. Unatakiwa kusema:

“Ee Allaah! Usininyime uombezi wa Mtume wako! Ee Allaah! Nifanye nipate uombezi wake.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) baada ya kufa kwake haombwi kitu. Ni mamoja iwe uombezi au kitu kingine. Kuwaomba vitu maiti baada ya kufa kwao ni shirki kubwa.

[1] al-Bukhaariy (7072), Muslim (193), Ibn Maajah (4312), Ahmad (03/116) na ad-Daarimiy (52).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 87
  • Imechapishwa: 18/01/2017