57. Radd tatu kwa yule mwenye kumuomba Mtume uombezi

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Akisema:

“Kwa hakika Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kapewa uombezi na mimi naomba kile alichompa Allaah.” Jibu ni kuwa:

“Ni kweli kuwa Allaah kampa uombezi, lakini amekukataza hili [yaani kuomba mtu mwengine isipokuwa Yeye]. Amesema:

فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Basi msiombe yeyote pamoja na Allaah.” (72:18)

Ikiwa utamuomba Allaah akupe uombezi wa Mtume Wake, basi tii maneno Yake:

فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Basi msiombe yeyote pamoja na Allaah.”

Isitoshe uombezi wamepewa wengine zaidi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Imesihi ya kwamba Malaika, mawalii na watoto waliokufa kabla ya kubaleghe watashufaia. Utasema ya kwamba: “Kwa vile Allaah kawapa uombezi, basi hivyo nitauomba kutoka kwao?” Ukisema hivyo, utakuwa umerejea katika kuwaabudia watu wema ambao Allaah amewataja katika Kitabu Chake. Na ukisema: “Hapana”, maneno yako yanakuwa yamebatilika: “Allaah kawapa uombezi na mimi ninaomba kile alichowapa Allaah.”

MAELEZO

Mshirikina ambaye anamuomba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema kuwa Allaah amempa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) haki ya kuombea na kwamba yeye anaiomba kutoka kwao, anajibiwa kwa njia tatu:

1 – Allaah amempa uombezi lakini amekukataza kumuomba mwengine asiyekuwa Yeye. Amesema:

فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Basi msiombe yeyote pamoja na Allaah.”

2 – Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amempa haki ya kuombea, lakini pamoja na hivyo hatoombea (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pasi na idhini ya Allaah. Wala hatumuombea isipokuwa yule ambaye Allaah yuko radhi naye. Allaah hayuko radhi na mshirikina na hivyo hatoidhinisha aombewe. Amesema (Ta´ala):

وَلَا يَشْفَعُونَ إِلَّا لِمَنِ ارْتَضَىٰ

“Na wala hawamuombei uombezi yeyote isipokuwa kwa yule ambaye Amemridhia.” (21:28)

3 – Allaah (Ta´ala) amewapa haki ya kuombea wengine zaidi ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Malaika watashufaia. Watoto waliokufa kabla ya kubaleghe watashufaia. Mawalii watashufaia. Muulize:

“Utawaomba uombezi watu hawa pia?”

Endapo atatoa jibu la kukataa, maoni yake yatakuwa yamebatilika. Akitoa jibu la kuitikia, atakuwa amerudi katika maoni ya kuwaabudia watu wema.

Jengine ni kwamba mshirikina huyu anachokusudia sio kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amwombee. Lau kama kweli anakusudia hilo, basi angelisema:

“Ee Allaah! Mfanye Mtume Wako Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anishufaie.”

Hata hivyo anamuomba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) moja kwa moja. Kumuomba asiyekuwa Allaah ni shirki kubwa yenye kumtoa mtu katika Uislamu. Ni vipi basi mtu huyu ambaye anawaomba wengine badala ya Allaah atataka ashufaiwe mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala)?

Mtunzi (Rahimahu Allaah) amesema:

“Imesihi ya kwamba Malaika, mawalii na watoto waliokufa kabla ya kubaleghe watashufaia… “

Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kuwa Allaah (´Azza wa Jall) atasema:

“Malaika wameshufaia. Mitume wameshufaia. Waumini wameshufaia.”[1]

Mtunzi (Rahimahu Allaah) amesema:

“… na watoto waliokufa kabla ya kubaleghe watashufaia… “

Abu Hurayrah ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Hakuna muislamu yeyote atayefisha watoto watatu aguswe na Moto, isipokuwa ni kwa lengo tu la kutekeleza kiapo.”[2]

Imepokelewa na al-Bukhaariy. Vilevile amepokea Hadiyth nyingine kutoka kwake na kutoka kwa Abu Sa´iyd al-Khudriy inayosema:

“… ambaye hajabaleghe.”[3]

[1] Muslim (302).

[2] al-Bukhaariy (1251).

[3] al-Bukhaariy (1250).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 70-71
  • Imechapishwa: 24/11/2023