Mfungaji anatakiwa kujiepusha pia na usengenyi. Nako ni kule kumsema nduguyo kwa yale anayoyachukia nyuma ya mgongo wake. Ni mamoja umemsema kwa yale anayoyachukia kuhusu maumbile yake, kama mfano wa kiguru, chongo na kipofu ukasema kwa njia mbaya na ya kumtia kasoro, au kwa kitu anachokichukia katika tabia yake, kama kwa mfano kusema kuwa ni mpumbavu, mjinga, fasiki na mfano wake. Haijalishi kitu analo hilo unalomsema au hana. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliulizwa kuhusu usengenyi ambapo akasema:

“Ni kumsema nduguyo kwa yale anayoyachukia.” Kukasemwa: “Unaonaje ikiwa ndugu yangu huyo yuko na hicho ninachomsemea?” Akasema: “Akiwa na hicho unachomsema basi umemsengenya. Asipokuwa na hicho unachomsema basi umemzulia.”

Ameipokea Muslim.

Allaah amekataza usengenyi ndani ya Qur-aan na akafananisha kitendo hicho na jambo baya kabisa. Amefananisha kitendo hicho na mwanamme anayekula nyama ya nduguye ambaye ameshakufa. Amesema (Ta´ala):

وَلَا يَغْتَب بَّعْضُكُم بَعْضًا ۚ أَيُحِبُّ أَحَدُكُمْ أَن يَأْكُلَ لَحْمَ أَخِيهِ مَيْتًا فَكَرِهْتُمُوهُ

“Na wala wasisengenyane baadhi yenu wengineo. Je, anapenda mmoja wenu kula nyama ya nduguye aliyekufa? Mnalichukia hilo!”[1]

Vilevile Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameeleza kuwa usiku ambao alipandishwa mbinguni aliwapitia watu wenye kucha kucha za shaba wakijichana nyuso zao na vifua vyao.” Akasema: “Ni kina nani hawa, ee Jibriyl?” Akasema: “Hawa ni watu ambao wamekula nyama za watu na kuwavunjia heshima zao.

Ameipokea Abu Daawuud.

[1] 49:12

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 70-71
  • Imechapishwa: 21/04/2021