56. Makatazo ya muislamu kusimamia na kuandaa maziko ya kafiri

2- Miongoni mwa mambo yanayopelekea katika kuwakufurisha makafiri ni kwamba mshirikina na kafiri wanapokufa, basi muislamu asisimamie maziko yake. Isipokuwa akikosa ambao watamzika katika makafiri wenzake. Katika hali hiyo achimbiwe shimo na kutupwa ndani yake na wala asizikwe katika makaburi ya waislamu. Waislamu hawatakiwi kusimamia maziko ya makafiri; wasimuoshe, wasimvike sanda, wasimbebe, wasihudhurie kuzikwa kwake na wala asizikwe katika makaburi ya waislamu. Amesema (Ta´ala):

وَلَا تُصَلِّ عَلَىٰ أَحَدٍ مِّنْهُم مَّاتَ أَبَدًا وَلَا تَقُمْ عَلَىٰ قَبْرِهِ ۖ إِنَّهُمْ كَفَرُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ وَمَاتُوا وَهُمْ فَاسِقُونَ

”Wala kamwe usimswalie yeyote miongoni mwao akifa na wala usisimame kaburini kwake [kwa ajili ya kumuombea]; kwani hakika wao wamemkanusha Allaah na Mtume Wake na wakafa hali wao ni mafasiki.” (at-Tawbah 09:84)

Muislamu hatakiwi kuandaa maziko ya makafiri na wala wasizikwe katika makaburi ya waislamu.

Ama kuhusu kumtembelea mgonjwa katika makafiri, ikiwa lengo ni kwa ajili ya kumlingania katika dini ya Allaah, basi muislamu anaweza kumtembelea kafiri na akamlingania katika dini ya Allaah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alienda kumtembelea myahudi na akamlingania katika Uislamu na akafa katika Uislamu na akashuhudia ya kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah[1]. Isitoshe Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alienda kumtembelea ami yake Abu Twaalib katika hali ya kukata roho na akamwambia:

“Ewe ami yangu! Sema “Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah.”[2]

Ikiwa lengo la kumtembelea kafiri ambaye ni mgonjwa ni kwa ajili ya kumlingania katika Uislamu, basi hapana ubaya wowote. Ama akishakufa basi haifai kwa muislamu kumsimamia, japokuwa atakuwa ni katika watu wa karibu sana naye, hata akiwa ni baba yake. Pindi Abu Twaalib alipokufa katika ukafiri Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakusimamia wala kuyaandaa maziko yake. Alichofanya ni kumuamrisha mtoto wake ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) kumfukia ndani ya ardhi na wala asiachwe juu ya ardhi ili asiwaudhi watu[3].

[1] Ameipokea al-Bukhaariy (1356), Abu Daawuud (5095), an-Nasaa´iy katika “al-Kabriy” (7458), Ahmad (13977) kupitia kwa Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh).

[2] al-Bukhaariy (1360) na Muslim (39).

[3] Ameipokea Abu Daawuud (3214) na an-Nasaa´iy (2006). Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 85-86
  • Imechapishwa: 26/09/2018