Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:
Baada ya mtihani huu, kuna ima neema au adhabu mpaka kitaposimama Qiyaamah kikubwa. Roho zitarudishwa kwenye miili. Qiyaamah ambacho Allaah (Ta´ala) amekielezea ndani ya Kitabu Chake na kupitia ulimi wa Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wakaafikiana juu yake waislamu, kitasimama. Watu watatoka ndani ya makaburi yao, wakiwa peku, uchi, wasiotahiriwa[1], wasimame mbele ya Mola wa walimwengu. Jua litajongezwa karibu yao na jasho zao zitafikia vinywa vyao [2].
MAELEZO
Baada ya hapo ndipo kutasimama Qiyaamah kikubwa. Haya yatatokea baada ya mtihani [wa ndani ya kaburi ambapo] mwanaadamu huwa ima katika neema au adhabu. Muumini anakuwa katika neema ambapo roho yake inahamishwa kupelekwa Peponi. Kafiri roho yake inahamishwa kupelekwa Motoni. Amesema (Subhaanah) kuhusu watu wa Fir´awn walioko Motoni:
النَّارُ يُعْرَضُونَ عَلَيْهَا غُدُوًّا وَعَشِيًّا ۖ وَيَوْمَ تَقُومُ السَّاعَةُ أَدْخِلُوا آلَ فِرْعَوْنَ أَشَدَّ الْعَذَابِ
“Wanadhihirishiwa Moto asubuhi na jioni, na Siku itakayosimama Qiyaamah [itasemwa]: “Waingizeni watu wa Fir’awn katika adhabu kali kabisa.” (40:46)
Hapa ndipo kitakuwa kimesimama Qiyaamah kikubwa na watu watoke ndani ya makaburi yao peku, uchi na bila ya kutahiriwa. Allaah atawafufua hali ya kuwa amewarudishia miili yao. Watakuwa kama walivyoumbwa mara ya kwanza.
[1] al-Bukhaariy (3349) na Muslim (2860).
[2] Muslim (2864).
- Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
- Tarjama: Firqatunnajia.com
- Marejeo: Sharh al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah, uk. 84-85
- Imechapishwa: 28/10/2024
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window)
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window)
- Click to print (Opens in new window)
- Click to email a link to a friend (Opens in new window)
- Click to share on Facebook (Opens in new window)
- Click to share on Twitter (Opens in new window)
- Click to share on Pocket (Opens in new window)