Imaam Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah) amesema:

Imani ni kutamka kwa ulimi, matendo ya viungo na kuamini moyoni. Inazidi kwa utiifu na inapungua kwa maasi. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَ ۚ وَذَٰلِكَ دِينُ الْقَيِّمَةِ

“Hawakuamrishwa jengine isipokuwa wamwabudu Allaah hali ya kumtakasia Yeye dini kwa kujiengua na shirki na kuelemea Tawhiyd, na wasimamishe swalah na watoe zakaah – na hiyo ndiyo dini iliyosimama imara.”[1]

Kafanya kumwabudu Allaah (Ta´ala), kuutakasa moyo, kusimamisha swalah na kutoa zakaah, yote hayo yanaingia katika dini. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Imani ni tanzu sabini na kitu. Ilio juu kabisa ni kusema “nashuhudia ya kwamba hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah… ” na ilio chini ni kuondoa chenye kudhuru njiani.”[2]

Amefanya kutamka na kutenda vyote vinaingia katika katika imani. Amesema (Ta´ala):

زَادَتْهُمْ إِيمَانًا

”Huwazidishia imani.”[3]

لِيَزْدَادُوا إِيمَانًا مَّعَ إِيمَانِهِمْ

”Ili awazidishie imani pamoja na imani zao.”[4]

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atatolewa ndani ya Moto yule aliyesema “hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah” na moyoni mwake mna imani kiasi cha punje ya ngano, mbegu ya haradali au vumbi nafaka.”[5]

Ameifanya imani kuwa inatofautiana.

MAELEZO

Imani kilugha ni kule kusadikisha.

Imani kiistilahi ni kutamka kwa ulimi, matendo ya viungo na kuamini moyoni. Mfano wa kutamka ni kusema “hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah”. Mfano wa matendo ni Rukuu´. Mfano wa kuamini moyoni ni kumwamini Allaah, Malaika Wake na mengineyo katika yale ambayo ni lazima kuyaamini. Dalili juu ya kwamba haya ni imani ni maneno Yake (Ta´ala):

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَ ۚ وَذَٰلِكَ دِينُ الْقَيِّمَةِ

“Hawakuamrishwa jengine isipokuwa wamwabudu Allaah hali ya kumtakasia Yeye dini kwa kujiengua na shirki na kuelemea Tawhiyd, na wasimamishe swalah na watoe zakaah – na hiyo ndiyo dini iliyosimama imara.”

Amefanya kule kumtakasia Allaah matendo, swalah na zakaah ni sehemu ya dini.

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Imani ni tanzu sabini na kitu. Ilio juu kabisa ni kusema “nashuhudia ya kwamba hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah… ” na ilio chini ni kuondoa chenye kudhuru njiani.”

Ameipokea Muslim kwa tamko lisemalo:

“Bora yake ni kusema “nashuhudia ya kwamba hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah.”

Msingi wake ni katika “as-Swahiyh” mbili[6].

[1] 98:05

[2] al-Bukhaariy (09) na Muslim (35).

[3] 08:02

[4] 48:04

[5] al-Bukhaariy (44) na Muslim (193).

[6] Muslim (35, 58) na al-Bukhaariy (09).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 99
  • Imechapishwa: 07/11/2022