2 – Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah):

“Jibu la Maalik ni mojawapo ya majibu bora na kamilifu ambayo yametolewa juu ya mada hiyo. Kwa sababu kwanza yanatupilia mbali kumfanyia namna, pili kumthibitishia Kulingana juu ambako kunafahamika. Wanazuoni wameyatilia umuhimu masimulizi yake, kuyakubali na kuyaona kuwa ni mazuri.”[1]

Amesema tena:

”Watu wameyapokea masimulizi haya kwa kuyakubali. Hakuna yeyote katika Ahl-us-Sunnah aliyeyakataa.”[2]

Amesema tena:

“Imepokelewa kupitia njia kadhaa kwamba bwana mmoja alimuuliza Maalik:

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

”Mwingi wa rehema amelingana juu ya ´Arshi.”[3]

Amelingana vipi?” Maalik akaanza kutokwa na jasho ambapo akajibu: “Kulingana juu kunatambulika na namna haitambuliki. Ni wajibu kuamini jambo hilo na kuuliza juu yake ni Bid´ah. Mimi sikuoni vingine isipokuwa mtu muovu.” Kisha akaamrisha atolewe nje.

Jibu kama hili limethibiti pia kutoka kwa Rabiy’ah, ambaye ni mwalimu wake Maalik. Jibu hili limepokewa pia kutoka kwa Umm Salamah (Radhiya Allaahu ́anhaa), kutoka kwake mwenyewe na kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hata hivyo cheni yake ya wapokezi si yenye kutegemewa. Vivyo hivyo maneno ya maimamu wote yanaenda sambamba na maneno ya Maalik, kwamba hatujui namna ya Kulingana Kwake juu kama ambavo pia hatujui namna ilivyo dhati Yake. Lakini tunajua ile maana iliyofahamishwa na mazungumzo. Tunajua maana ya Kulingana juu lakini hatujui namna yake. Vivyo hivyo tunajua maana ya Kushuka lakini hatujui namna yake. Tunajua maana ya Kusikia, Kuona, Ujuzi na Uwezo na wala hatujui namna ya sifa hizo. Vilevile tunajua maana ya Huruma, Ghadhabu, Kuridhia na Kucheka na wala hatujui namna ya sifa hizo.”[4]

[1] Sharh Hadiyth-in-Nuzuul, uk. 310.

[2] Majmuu´-ul-Fataawaa (13/309).

[3] 20:05

[4] Sharh Hadiyth-in-Nuzuul, uk. 218-219.

  • Muhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Allaamah ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad al-Badr
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Athar al-Mash-huur ´an-il-Imaam Maalik fiy Swifat-il-Istiwaa’, uk. 80
  • Imechapishwa: 16/12/2025