55. Uombezi kati ya viumbe wao kwa wao


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Naamini uombezi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kwamba ndiye mwombezi wa kwanza na ndiye wa kwanza atakayekubaliwa uombezi wake.

MAELEZO

Naamini uombezi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – Maana yake ni kwamba nasadikisha na naitakidi uombezi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Shufwa ni kitu kilichozidi moja. Moja huitwa witr na mbili huitwa shufwa. Amesema (Ta´ala):

وَالشَّفْعِ وَالْوَتْرِ

“Naapa kwa shufwa na witr.”[1]

Kwa hiyo shufwa ni chenye kuzidi moja. Witr ni moja. Hii ni maana ya kilugha.

Ama kiistilahi uombezi maana yake kunakusudiwa kuwakalia katikati wahitaji katika kutatua haja zao kutoka kwa Anayemiliki. Kwa sababu mwenye kuombwa haja hiyo ni mmoja tu. Akiingia katikati mwengine na ikawa shufwa baada ya kwamba alikuwa mmoja ndio maana ikaitwa “shufwa”. Baadhi ya wengine wanasema kuwa maana yake ni kuomba kheri kutoka kwa mwengine.

Uombezi umegawanyika aina mbili:

1- Uombezi mbele ya Allaah.

2- Uombezi mbele ya viumbe.

Uombezi mbele ya viumbe umegawanyika sampuli mbili:

1- Uombezi mzuri.

2- Uombezi mbaya. Amesema (Ta´ala):

مَّن يَشْفَعْ شَفَاعَةً حَسَنَةً يَكُن لَّهُ نَصِيبٌ مِّنْهَا ۖ وَمَن يَشْفَعْ شَفَاعَةً سَيِّئَةً يَكُن لَّهُ كِفْلٌ مِّنْهَا

“Atakayeombea uombezi mzuri atapata fungu lake katika hayo. Na atakayeombea uombezi mbaya atapata sehemu katika hayo.”[2]

Ikiwa uombezi ni kwa ajili ya kufikia kitu cha halali na kitu chenye manufaa basi huo ni uombezi mzuri. Ni kwa mfano ukatumia cheo chako mbele ya mfalme au mtawala katika kutatua haja ya kaka yako. Hivyo ukawaombea ndugu zako katika kufikia maombi yao yanayoruhusu na maslahi yao yenye manufaa. Huu ni uombezi mzuri. Kwa sababu ni jambo linaingia katika wema na kusaidiana:

“Allaah ni Mwenye kumsaidia mja muda wa kuwa mja ni mwenye kumsaidia ndugu yake.”[3]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Fanyeni uombezi mtapewa ujira.”[4]

Ndani yake kuna ubainifu kwamba uombezi mzuri mtu analipwa thawabu kwao. Kwani ndani yake kuna manufaa kwa wahitaji.

Ama kuhusu uombezi mbaya ni kufanya uombezi juu ya jambo la haramu. Kwa mfano kufanya uombezi juu ya kuangusha adhabu moja wapo ya Allaah ya Kishari´ah kwa yule ambaye inamstahikia kwamba asisimamishiwe adhabu hiyo. Huu ndio uombezi wa haramu na amelaaniwa mwenye kufanya hivo. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Adhabu ya Kishari´ah ikimfikia mtawala basi Allaah amemlaani mwombezi na mwombewaji.”[5]

Wakati Usaamah bin Zayd alipotaka kumuombea msamaha mwanamke ambaye anastahiki adhabu ya kuiba na hilo likawa gumu juu ya kabila lake ambapo wakamwendea Usaamah aende kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumuombea msamaha asikatwe mkono wake. Usaamah akamfanyia maombezi na akazungumza na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akakasirika sana na akasema:

“Hivi unafanya uombezi juu ya adhabu katika adhabu za Allaah? Hakika kilichowafanya kuangamia waliokuwa kabla yenu ni kwamba walikuwa anapoiba katika wao mtu mtukufu, basi humwacha na anapoiba mtu mnyonge, basi wanamsimamishia adhabu ya Kishari´ah. Ninaapa kwa Allaah! Laiti Faatwimah, msichana wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ataiba basi nitaukata mkono wake.”[6]

Imepokelewa katika Hadiyth:

“Allaah amlaani mwenye kumsaidia mzushi.”[7]

Kumsaidia maana yake amemlinda asisimamishiwe juu yake hukumu ya Kishari´ah.

Kwa hiyo uombezi mbaya ni ule unaokuwa juu ya kitu cha haramu.

[1] 89:03

[2] 04:85

[3] Muslim (2699) kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh).

[4] al-Bukhaariy (2432) na Muslim (2627) kupitia kwa Abu Muusa (Radhiya Allaahu ´anh).

[5] ad-Daaraqutwniy katika ”as-Sunnah” (03/205 nambari. 364), at-Twabaraaniy katika ”al-Awsatw” (02/380 nambari. 2284) kupitia kwa az-Zubayr bin al-´Awwaam. Tazama ”Fath-ul-Baariy” (12/87-88).

[6] al-Bukhaariy (3475) na Muslim (1688) kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anh).

[7] Muslim (1978) kupitia kwa ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 81-82
  • Imechapishwa: 09/04/2021