Miongoni mwa wafungaji wako ambao wanapuuza swalah ya mkusanyiko licha ya kuwa ni wajibu juu yao. Allaah ameiamrisha ndani ya Kitabu Chake pale aliposema:

وَإِذَا كُنتَ فِيهِمْ فَأَقَمْتَ لَهُمُ الصَّلَاةَ فَلْتَقُمْ طَائِفَةٌ مِّنْهُم مَّعَكَ وَلْيَأْخُذُوا أَسْلِحَتَهُمْ فَإِذَا سَجَدُوا

“Utapokuwa upo kati yao ukawaswalisha, basi lisimame kundi miongoni mwao pamoja nawe na wabebe silaha zao… “

Bi maana wakakamilisha swalah yao:

فَلْيَكُونُوا مِن وَرَائِكُمْ وَلْتَأْتِ طَائِفَةٌ أُخْرَىٰ لَمْ يُصَلُّوا فَلْيُصَلُّوا مَعَكَ وَلْيَأْخُذُوا حِذْرَهُمْ وَأَسْلِحَتَهُمْ ۗ وَدَّ الَّذِينَ كَفَرُوا لَوْ تَغْفُلُونَ عَنْ أَسْلِحَتِكُمْ وَأَمْتِعَتِكُمْ فَيَمِيلُونَ عَلَيْكُم مَّيْلَةً وَاحِدَةً ۚ وَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ إِن كَانَ بِكُمْ أَذًى مِّن مَّطَرٍ أَوْ كُنتُم مَّرْضَىٰ أَن تَضَعُوا أَسْلِحَتَكُمْ

“… watakaposujudu basi wawe nyuma yenu [kuwalinda] na lije kundi jengine ambalo halikuswali na liswali pamoja nawe, nao wachukue tahadhari na silaha zao. Wale waliokufuru wanatamani iwapo mtaghafilika na silaha zenu na vifaa vyenu wakuvamieni mvamio papohapo. Na wala si dhambi kwenu ikiwa mna maudhiko kutokamana na mvua au mkiwa wagonjwa kuweka chini silaha zenu.”[1]

Allaah akaamrisha kuswali swalah ya mkusanyiko katika hali ya mapigano na khofu. Hivyo katika hali ya amani na utulivu ina haki zaidi. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza:

“Kuna bwana mmoja kipofu alisema: “Ee Mtume wa Allaah! Mimi sina mwelekezaji wa kuniongoza kwenda msikitini. Akamruhusu. Wakati alipompa mgongo akamwita ambapo akasema: “Je, unasikia wito wa swalah?” Akasema: “Ndio.” Akasema: “Basi imewajibika.”

Ameipokea Muslim.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakumruhusu kuacha kwake swalah ya mkusanyiko pamoja na kwamba ni kipofu na hana wa kumwongoza.

Mtu kuiacha swalah pamoja na kuipoteza ameiharamishia nafsi yake kheri nyingi kwa kupata matendo mema mengi. Swalah ya mkusanyiko ni yenye kulipwa kwa wingi. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swalah ya mkusanyiko inashinda anayeswali peke yake kwa ngazi ishirini na saba.”

Pia amekosa manufaa ya kukusanyika yanayopatikana kwa kule kukusanyika kwa waislamu juu ya swalah katika kupendana, kuungana, kumfunza mjinga, kumsaidia muhitaji na mengineyo.

Yule mwenye kuacha swalah ya mkusanyiko ameiweka nafsi yake katika khatari ya adhabu na kujifananisha na wanafiki. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swalah ngumu kwa wanafiki ni swalah ya ´ishaa na swalah ya fajr. Lau wangelijua yaliyomo [katika swalah hizo mbili] basi wangeziendea ijapo kwa kutambaa. Nimetamani niamrishe kusimamishwe swalah na kukimiwe ambapo nimwamrishe mtu awaswalishe watu kisha niondoke na kikosi cha watu wakiwa na kuni kuwaendea watu wasiohudhuria swalah nikawatilia moto nyumba zao.”

Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema:

“Anayependa kukutana Allaah kesho hali ya kuwa ni muislamu basi azichunge swalah hizi pale zinaponadiwa. Hakika Allaah amemuwekea Shari´ah Mtume wenu mwenendo wa uongofu. Nazo ni katika mwenendo wa uongofu. Si vyenginevyo tulikuwa tunaona yule mwenye kuziacha ni mnafiki ambaye unafiki wake ni wenye kujulikana. Mtu alikuwa akiletwa hali ya kuwa amebebwa kati ya wanamme wawili mpaka anasimamishwa katikakati ya safu.”

Miongoni mwa wafungaji wako ambao wanapindukia wanalala na kuacha kuswali ndani ya wakati wake. Hii ni dhambi kubwa na aina khatari zaidi ya kuzipoteza swalah. Hali imefikia kiasi cha kwamba wanachuoni wengi wamesema kuwa yule mwenye kuchelewesha swalah mpaka ukatoka wakati wake pasi na udhuru unaokubalika kidini haikubaliwi ijapo ataswali mara mia. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote atakayefanya kitendo kisichoafikiana na dini yetu atarudishiwa mwenyewe.”

Ameipokea Muslim.

Kuswali nje ya wakati wake ni kitu kisichoafikiana na dini ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hivyo inakuwa ni yenye kurudishwa na si yenye kukubaliwa.

[1] 04:102

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 67-69
  • Imechapishwa: 19/04/2021