Swali: Baadhi ya maimamu wanarefusha du´aa ya Qunuut na hawasomi katika Tarawiyh isipokuwa kurasa nne peke yake kutoka ndani ya Qur-aan. Unasameje juu ya hilo?

Jibu: Ni kweli kwamba baadhi ya maimamu wanarefusha Qunuut na wakati huohuo wanapumbaa kuizingatia Qur-aan, kuwaidhika nayo na kunyenyekea kwa Allaah (Ta´ala). Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

لَوْ أَنزَلْنَا هَـٰذَا الْقُرْآنَ عَلَىٰ جَبَلٍ لَّرَأَيْتَهُ خَاشِعًا مُّتَصَدِّعًا مِّنْ خَشْيَةِ اللَّـهِ

“Lau Tungeliiteremsha Qur-aan hii juu ya mlima, basi ungeuona ni wenye kunyenyekea wenye kupasukapasuka kutokana na khofu ya Allaah kutokana na kumuogopa Allaah.”[1]

Inatupasa sote kuisoma Qur-aan kwa mazingatio, kunyenyekea na kuizingatia, kuwaidhika na mafunzo yake na kuisoma kwa sauti nzuri na kati na kati. Kwa ajili hiyo ni katika makosa na kuiacha Sunnah yale yanayofanywa na baadhi ya maimamu pale wanapokimbiza mbali na Qur-aan na kuharibu kisomo chake. Baadhi pengine wasisome isipokuwa baadhi ya Aayah na baadaye wanaharakia kwenda katika Rukuu´ na Sujuud kwa njia inayoharibu nguzo ya utulivu. Yote hayo kwa ajili ya kurefusha du´aa. Utawaona wanazikariri baadhi ya du´aa na wanajifanya kulia, jambo ambalo linapelekea kurefusha swalah na kuwatia waswaliji kwenye uzito na ugumu, na khaswa wale watuwazima. Matokeo yake wanajutia kuswali na kuchoshwa na du´aa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah hachoki mpaka nyinyi mchoke. Hakika miongoni mwa matendo yanayopendeza zaidi kwa Allaah ni yale yenye kudumu ijapo yatakuwa machache.”[2]

Baadhi wanaweka theluthi ya wakati wa swalah katika du´aa. Wengine wanaweka nusu ya wakati katika du´aa. Baadhi ya wengine pengine wakaenda zaidi ya hivo. Haya yote yanaenda kinyume na Sunnah. Ni kwa nini kusirefushwe kisomo cha Qur-aan, Rukuu´ na Sujuud? Ni kwa nini badala yake mtu asilie mahali hapo? Hili ndio linaloafikiana na Sunnah. Hivo ndivo alivoswali Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio ruwaza yetu njema.

Mbali na urefushaji wa du´aa kuna khatari ya kuomba du´aa zisizokuwa na msingi. Pengine kukaombwa kitu kisichowezekana au zenye dhambi. Huku ni kuchupa mpaka katika du´aa. Wako wanaoomba kwa kusema:

“Ee Allaah! Hakika mimi nimekutii kama Ulivyoniamrisha.”

Hayo hayakusemwa hata na Abu Bakr as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ndiye kiumbe bora na mwenye kumcha Allaah zaidi baada ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Vipi tunaweza kusema kitu kama hicho licha ya mapungufu na madhambi yetu? Hivi kweti sisi tunamtii Allaah katika yale yote anayotuamrisha? Hakuna yeyote katika sisi anaweza kuitikia. Kila mmoja anaijua nafsi yake. Hivi kweli tunaweza kusema kuwa tumeyaeupuka yale yote ambayo Ametukataza? Haijuzu kwetu kusema namna hiyo. Allaah (Subhaanahu wa Ta´aal) anatujua sisi zaidi tunavyozijua nafsi zetu. Anayajua yale yote tunayoyafanya na kuyasema. Hakuna chochote kinachofichikana Kwake. Kila mmoja katika sisi anajua yale mapungufu alionayo inapokuja katika yale mambo ya wajibu na kuyaepuka makatazo. Kwa hiyo tumche Allaah juu ya nafsi zetu na tulazimiane na du´aa za kinabii. Hebu tulazimiane na vitabu vilivyosalimika kama mfano wa “Riyaadh-us-Swaalihiyn” au “Tuhfat-ul-Akhyaar” cha Ibn Baaz. Yule mwenye kurejea huko atafaidika sana na atamwomba Allaah kwa du´aa fupi zenye maana pana. Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) mtumishi wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), amesema:

“Du´aa ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiomba kwa wingi:

رَبَّنَا آتِنَا فِي الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِي الآخِرَةِ حَسَنَةً وَقِنَا عَذَابَ النَّارِ

“Ee Mola! Tupe mazuri ya dunia na mazuri ya Aakhirah na tukinge na adhabu ya Moto.”[3]

Alikuwa anaweza kuiunganisha na du´aa nyingine. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Ee Allaah! Niseme nini nikiuafiki usiku wa Qadar?” Akasema: “Sema:

اللَّهُمَّ إِنَّكَ عَفُوٌّ تُحِبُّ الْعَفْوَ فَاعْفُ عَنِّي

“Ee Allaah! Hakika Wewe ni mwingi wa kusamehe. Hivyo basi, nisamehe.”[4]

[1] 59:21

[2] Ahmad (26308).

[3] al-Bukhaariy (6389) na Muslim (2690).

[4] at-Tirmidhiy (3513), Ibn Maajah (3850) na Ahmad (25423). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaamiy´” (4423).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah Aalush-Shaykh
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Min Fataawaas-Swiyaam, uk. 42-44
  • Imechapishwa: 07/04/2022