Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

84 – Hatumkatii yeyote katika wao Pepo wala Moto. Hatushuhudii juu yao ukafiri, shirki wala unafiki muda wa kuwa haijatudhihirikia chochote katika mambo hayo. Tunaziacha siri zao kwa Allaah (Ta´ala).

MAELEZO

Hatumthibitishii yeyote Pepo, isipokuwa wale Maswahabah kumi waliobashiriwa Pepo, ´Abdullaah bin Salaam na wengineo. Hakika sisi tunawashuhudia Pepo kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewashuhudia. Vivyo hivyo mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) ametamka hivo waziwazi huko mbele ya kitabu.

Miongoni mwa ujinga na upotevu wa baadhi ya watunzi wa vitabu, ni kumtuhumu ´Abdullaah bin Salaam juu ya uyahudi wake kabla ya kuingia katika Uislamu – licha ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemshuhudia kuingia Peponi[1]. Laiti ningejua kuna tofauti gani kati ya ambaye alikuwa myahudi kisha baadaye akasilimu na ambaye alikuwa mshirikina kisha baadaye akasilimu. Kwa masikitiko makubwa inahusiana na mori za kitaifa za kipindi cha kikafiri. Bila shaka, kuna tofauti. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameeleza kuwa watu aina tatu wanalipwa thawabu mara mbili, ambapo akataja mmoja katika wao ni mtu katika watu wa Kitabu ambaye amemuamini Mtume wake, baadaye akakutana na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akamuamini, akamfuata na kumsadikisha[2]. Hata hivyo mshirikina ambaye ameingia katika Uislamu anapata thawabu mara moja.

[1] al-Bukhaariy.

[2] al-Bukhaariy (3011) na Muslim (153).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah – Sharh wa Ta´liyq, uk. 76-77
  • Imechapishwa: 08/10/2024