Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

85 – Hatuoni kufaa kumsimamishia upanga yeyote katika ummah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) isipokuwa yule ambaye umemuwajibikia upanga. Hatuoni kufaa kuwafanyia uasi viongozi na watawala wetu hata wakidhulumu. Hatuombi du´aa dhidi yao. Hatuondoi mkono katika kuwatii. Tunaona kuwa kuwatii wao ni kumtii Allaah (´Azza wa Jall) ambako amefaradhisha muda wa kuwa hawajaamrisha maasi. Tunawaombea kutengemaa na kusalimika.

MAELEZO

Baada ya kutaja Hadiyth nyingi muhimu katika maelezo yake, akasema Ibn Abiyl-´Izz:

”Kuendelea kuwatii ingawa wanadhulumu, ni kwa sababu kuwafanyia uasi kunapelekea katika madhara makubwa kuliko yale madhara yanayopatikana ya unyanyasaji wao. Bali makosa yanasamehewa kwa kule kuwa na subira juu ya dhuluma zao. Allaah hakuwafanya watutawale isipokuwa ni kwa sababu ya ubaya wa matendo yetu. Mtu anavuna kile alichopanda. Kwa hivyo ni juu yetu kuomba msamaha, kutubu na kuyatengeneza matendo yetu. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَا أَصَابَكُم مِّن مُّصِيبَةٍ فَبِمَا كَسَبَتْ أَيْدِيكُمْ وَيَعْفُو عَن كَثِيرٍ

“Haukupateni katika msiba wowote basi ni kwa sababu ya yale yaliyochuma mikono yenu na anasamehe mengi.”[1]

وَكَذَٰلِكَ نُوَلِّي بَعْضَ الظَّالِمِينَ بَعْضًا بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ

”Na hivyo ndivyo Tunavyowafanya baadhi ya madhalimu kuwa marafiki wao kwa wao kwa yale waliyokuwa wakiyachuma.”[2]

Kwa hivyo ikiwa wananchi wanataka kuepuka dhuluma za watawala, basi wao wenyewe waache kwanza dhuluma.”[3]

Yanafahamisha kuwa njia pekee ya kuepuka dhuluma za watawala – watawala ambao wanatokana na ngozi yetu na wanazungumza lugha yetu – ni kwamba waislamu watubu kwa Mola wao na wazitengeneze ´Aqiydah zao na wazileee nafsi zao wao na familia zao juu ya Uislamu sahihi, kwa ajili ya kuhakikisha maneno Yake Allaah (Ta´ala):

إِنَّ اللَّـهَ لَا يُغَيِّرُ مَا بِقَوْمٍ حَتَّىٰ يُغَيِّرُوا مَا بِأَنفُسِهِمْ

“Hakika Allaah hayabadilishi yale yaliyoko kwa watu mpaka wao wenyewe kwanza wabadilishe yale yaliyomo katika nafsi zao.”[4]

Ameashiria hilo mmoja katika walinganizi wa leo pale aliposema:

”Isimamisheni dola ya Kiislamu ndani ya nyoyo zenu, itasimamishwa kwenye ardhi yenu.”

Kinyume na wanavyofikiri baadhi ya watu, suluhu haiko hata kidogo katika maasi ya kutumia silaha na mapinduzi ya kijeshi dhidi ya walio madarakani. Tukiacha kuwa njia hizo ni miongoni mwa njia zilizozuliwa za sasa, zinapingana vilevile na maandiko ya Shari´ah yanayoamrisha kujibadilisha sisi wenyewe kwanza. Ili kujenga nyumba, ni lazima kwanza kujenga msingi madhubuti ambao nyumba itasimama juu yake:

وَلَيَنصُرَنَّ اللَّـهُ مَن يَنصُرُهُ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَقَوِيٌّ عَزِيزٌِ

“Bila shaka Allaah atamnusuru yule mwenye kuinusuru dini Yake – hakika Allaah ni Mwenye nguvu asiyeshindikana.”[5]

[1] 42:30

[2] 6:129

[3] Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 543

[4] 13:11

[5] 22:40

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah – Sharh wa Ta´liyq, uk. 77-79
  • Imechapishwa: 08/10/2024