51. Radd juu ya utata wa kwanza: mawalii wa Allaah hakuna khofu juu yao

Mfano wa hilo, ni pale baadhi ya washirikina wanaposema:

أَلَا إِنَّ أَوْلِيَاءَ اللَّـهِ لَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ

”Tanabahi! Hakika mawalii wa Allaah hakuna khofu juu yao na wala hawatohuzunika.” (Yuunus 10 : 62)

au anasema ya kwamba uombezi ni haki au ya kwamba Mitume wana jaha mbele ya Allaah. Au akataja maneno kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anakitolea dalili kitu katika batili yake, ilihali wewe hufahamu maana ya maneno aliyoyataja. Mjibu kwa kumwambia: “Kwa hakika Allaah amesema katika Kitabu Chake ya kwamba wale ambao moyoni mwao mna upotofu wanaacha Aayah zilizo wazi na badala yake wanafuata Aayah zisizokuwa wazi.” Na katika yale niliyokutajia ya kwamba Allaah ametaja ya kwamba washirikina walikuwa wanakubali Rubuubiyyah na kukufuru kwao ilikuwa ni kwa kujikurubisha kwao kwa Malaika, Mitume, mawalii kwa kusema kwao:

هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ

”Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.” (Yuunus 10 : 18)

Hili ni jambo lililo wazi na bainifu na wala hawezi yeyote kubadilisha maana yake. Wewe mshirikina! Sielewi maana ya uliyoyataja katika Qur-aan au maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), lakini nina uhakika kabisa ya kwamba maneno ya Allaah hayagongani, na kwamba maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hayaendi kinyume na maneno ya Allaah. Na hili ni jibu zuri sana, lakini halifahamu isipokuwa yule ambaye Allaah amempa ufahamu. Hivyo, usilidharau. Kwa hakika (Ta´ala) anasema:

وَمَا يُلَقَّاهَا إِلَّا الَّذِينَ صَبَرُوا وَمَا يُلَقَّاهَا إِلَّا ذُو حَظٍّ عَظِيمٍ

”Na hawatopewa [sifa hii] isipokuwa wale waliosubiri na hapewi hayo isipokuwa mwenye fungu kubwa.” (al-Fuswswilat 41 : 35)

MAELEZO

Mmoja katika wanachuoni wa washirikina ambao wanawaabudu mawalii na wanaomba kutoka kwao msaada na uokozi akikwambia – kama ilivyo hivi sasa kwa waabudu makaburi kwa kutumia dalili ya kwamba Allaah (Jalla wa ´Alaa) anasema:

أَلَا إِنَّ أَوْلِيَاءَ اللَّـهِ لَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ

”Tanabahi! Hakika mawalii wa Allaah hakuna khofu juu yao na wala hawatohuzunika.” (10:62)

na kusema kuwa watu hawa ni mawalii na kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameeleza kuwa watu wema, mawalii na Mitume watamuombea, mjibu kwa kumwambia kuwa uombezi ni haki na ni jambo lisilokuwa na shaka. Lakini mambo ni kama alivyotaja Allaah ni lazima kutimie masharti mawili:

Ya kwanza: Muombeaji apewe idhini ya kuombea.

Ya pili: Muombewaji awe katika watu wa Tawhiyd.

Hapana shaka kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amewaahidi mawalii ya kwamba hawana shaka yoyote na kwamba hawatohuzunika. Lakini ni wepi mawalii? Je, mawalii ni kundi la watu maalum walio na vilemba na mavazi maalum au mawalii ni wale waliojengewa juu ya makaburi yao makuba? Mambo sivyo. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amewabainisha moja kwa moja ni kina nani baada ya Aayah hii pale aliposema:

الَّذِينَ آمَنُوا وَكَانُوا يَتَّقُونَ

“Wale ambao wameamini na wakamcha Allaah.” (10:63)

Kila muumini aliye na uchaji basi ni walii wa Allaah. Uwalii sio jambo lililokomeka kwa kundi maalum au watu maalum walio na mavazi maalum, alama maalum au juu ya makaburi yao kumejengwa makuba na yamepambwa. Walii ni kila muumini aliye na uchaji. Huyo ndiye walii wa Allaah kwa dalili ya Aayah hii. Uwalii unatofautiana kwa kutegemea na imani na kumcha Allaah. Kuna ambao ni mawalii wenye uwalii kamilifu. Kuna ambao ni mawalii chini ya hivo kwa kutegemea imani na uchaji wake. Uwalii haukukomeka tu na yale wanayodai kwa watu hawa au waliyomo ndani ya makaburi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Huenda mwenye nywele matifutifu anayefukuzwa milangoni lau atamuapia Allaah [amfanyie jambo fulani] angelimfanyia.”[1]

Walii anaweza kuwa hajulikani na wala hana nafasi mbele ya watu. Hili ni mosi.

Pili ikithibiti kweli kuwa ni walii wa Allaah (´Azza wa Jall) hakumpi kitu katika haki za uola wala chochote katika haki za Allaah. Kwa kuwa yeye ni kiumbe wa Allaah anayemuhitaji Mola Wake (´Azza wa Jall). Hamiliki katika amri chochote; haumbi na wala haruzuku. Haina maana kwamba mtu akiwa walii basi sisi tunafungamana naye, tunamdhalilikia haja zetu kwake, tunamtaka uokozi na kutafuta kutoka kwake. Allaah amesema:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa na anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa Amtakae.” (04:48)

وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا

“Mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe na chochote.” (04:36)

Haijalishi kitu sawa awe walii au mwengine. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) haridhii haya. Maana ya maneno Yake (Ta´ala):

أَلَا إِنَّ أَوْلِيَاءَ اللَّـهِ لَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ

”Tanabahi! Hakika mawalii wa Allaah hakuna khofu juu yao na wala hawatohuzunika.” (10:62)

haina maana kuwa wanamiliki kitu katika uola, kwamba wananufaisha au wanadhuru, wao ndio wenye kutoa uombezi na kadhalika. Hivyo ndivyo wanavyodhani wale wenye kuyaabudu makaburi.

Atayefungamana na mawalii na akaomba kutoka kwao uombezi ilihali ni maiti, akaomba kutoka kwao uokozi ilihali ni maiti, akaomba kutoka kwao wamtatulie matatizo yake ilihali wamo ndani ya makaburi yao, basi yeye ni katika wale washirikina wa mwanzo ambao Allaah amesema juu yao:

وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ

“Wanaabudu badala ya Allaah visivyowadhuru wala kuwanufaisha na wanasema: “Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.”” (10:18)

Wao wanasema kuwa hawaitakidi kwamba wanaumba na kuruzuku na kwamba eti wanawafanya tu kuwa wakati kati baina yao na Allaah kwa kuwa wao ni mawalii wa Allaah na upande mwingine wao wana mapungufu na madhambi. Kwa ajili hiyo wanasema kuwa watu hawa kwa wema wao, jaha yao na nafasi walionayo mbele ya Allaah wanawaombea. Ndipo Allaah akawaraddi kwa kusema:

سُبْحَانَهُ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ

“Utakasifu ni Wake na yuko juu kabisa kwa yale yote wanayomshirikisha.”” (10:18)

Ameita haya kuwa ni shirki. Amesema katika Aayah nyingine:

أَلَا لِلَّـهِ الدِّينُ الْخَالِصُ ۚ وَالَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّـهِ زُلْفَىٰ

“Tanabahi! Ni ya Allaah pekee dini iliyotakasika. Na wale waliojichukulia badala Yake walinzi [husema]: “Hatuwaabudu isipokuwa ili watukurubishe kwa Allaah ukaribio.” (39:03)

Hakuna kingine wanachotaka isipokuwa ni ukati kati mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Vinginevyo wao wanatambua ya kwamba Allaah ndiye Muumba, Mruzukaji, Muhuishaji na Mfishaji. Wanaitambua Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah kikamilifu kama Allaah alivyosema kuhusu wao. Hakuna kingine walichokusudia kwa kitendo chao hichi cha kuwaweka kati na kati waja wema hawa isipokuwa ni ili wawafikishe kwa Allaah. Kwa ajili hiyo ndio maana wakawawekea nadhiri, wakawachinjia na wakaomba uokozi kutoka kwao na kusema:

“Ee bwana wangu, niombee kwa Allaah! Fanya kadhaa!”

Haya ndio wanayoyasema kwenye makaburi. Je, haya yanatofautiana na yale wanayosema washirikina wa hapo kabla ambao (Jalla wa ´Alaa) amewaraddi kwa kusema:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي مَنْ هُوَ كَاذِبٌ كَفَّارٌ

“Hakika Allaah atahukumu baina yao katika yale waliyokhitilafiana. Hakika Allaah hamwongoi ambaye ni muongo kafiri.” (39:03)

Wamehukumiwa uongo na kufuru. Kitendo chao hichi ni kufuru na uongo. Katika Suurah “Yuunus” ameitakasa nafsi Yake kutokamana na hilo aliposema:

سُبْحَانَهُ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ

“Utakasifu ni Wake na yuko juu kabisa kwa yale yote wanayomshirikisha.”” (10:18)

Ameita kuwa ni shirki.

[1] Muslim (2622).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 70-72
  • Imechapishwa: 01/01/2017