Swali: Je, kuna dalili yoyote kutoka katika Qur-aan au Sunnah au maneno ya wanazuoni juu ya kwamba imamu anatakiwa kukhitimisha Qur-aan katika swalah ya Tarawiyh na mwishowe kumuomba du´aa Allaah na kumshukuru? Ni yepi mategemezi ya kitendo hichi?

Jibu: Du´aa baada ya kukhitimisha Qur-aan wameirithi waislamu kizazi baada ya kizazi. Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) – ambaye anatambulika kuifuata Sunnah na Maswahabah na Taabi´uun – ametaja alivomkuta Sufyaan Makkah na wanazuoni wengine katika miji ya Kiislamu namna wanavokhitimisha Qur-aan na wanasoma du´aa ya kukhitimisha Qur-aan baada yake. Kwa ajili hiyo haitakiwi kumsimanga yule anayefanya hivo. Vitabu vya wanazuoni vimejaa jambo hilo. Wanajengea hoja kwamba du´aa baada ya kukhitimisha Qur-aan hairudishwi. Ilikuwa ni miongoni mwa matendo ya Salaf watu kukusanyika na kuomba du´aa wakati wa kukhitimisha Qur-aan. Ibn ´Abbaas na wengine walikuwa wakiwakusanya wanafunzi zao wakati wa kukhitimisha Qur-aan nje ya swalah na wanasema kuwa mkusanyiko umezungukwa na baraka na du´aa ni yenye kuitikiwa. Walikuwa wanaona kuwa haina neno kukhitimisha Qur-aan katika swalah za sunnah na kwamba Salaf walifanya hivo. Midhali Salaf walifanya hivo, basi ni makosa kuonelea kuwa kitendo hicho ni batili, Bid´ah na kumkemea yule mwenye kufanya hivo. Wewe ukiwa si mwenye kukinai usifanye hivo. Usihudhurie. Kiigizo chetu sisi ni Salaf. Sio jambo lililozuliwa; ni jambo la kale na Salaf wakalitendea kazi. Wanazuoni wenye pupa juu ya Sunnah na kuepuka Bid´ah wamelizungumzia. Kwa ajili hiyo sionelei kusimangwa kitendo hicho.

Shaykh wetu ´Abdul-´Aziyz bin Baaz (Rahimahu Allaah) ni miongoni mwa watu waliokuwa wakiipupia na kuifuata sana Sunnah. Alikuwa akiswali nyuma ya maimamu wanaokhitimisha Qur-aan. Kipindi muheshimiwa fulani alipotunga kijitabu kinachokemea kitendo hicho na akamuomba Shaykh akipendekeze na kukiandikia dibaji, Shaykh akasema:

“Mimi mwenyewe nahudhuria kunapokhitimishwa Qur-aan na sionelei kuwa kitendo hicho kinaenda kinyume na Sunnah. Siwezi kusifu radd ya kitu ambacho mimi na waalimu wangu kabla yangu wanakihudhuria. Salaf wametaja kitendo hicho katika vitabu vyao, jambo ambalo linajulisha kuwa kitendo hicho kina msingi.”

Shaykh akakataa kupendekeza kijitabu hicho. Hoja yake ilikuwa kama kitendo hicho kingekuwa Bid´ah, basi angelilazimika kuzingatia vizazi vya kabla yake kama wazushi na wamepinda kuiacha haki. Wanazuoni watukufu wana maoni hayohayo juu ya kitendo hichi. Kitendo hicho ananasibishiwa pia Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah).  Ana kila haki. Kitendo hicho kina du´aa zilizopokelewa na hakina Bid´ah wala kuchupa mpaka katika du´aa. Pindi maimamu wanapomaliza Qur-aan yote, basi wanatakiwa kulazimiana na adabu na kujiepusha mbali na kuchupa mpaka katika du´aa. Wakishikamana na njia hii, basi nataraji kuwa hapana neno. Sisi pia tunakifanya kama maimamu wengine wote.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah Aalush-Shaykh
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Min Fataawaas-Swiyaam, uk. 40-41
  • Imechapishwa: 04/04/2022