Anas (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna ´Aqr katika Uislamu.”

Ameipokea Imaam Ahmad katika Hadiyth ndefu kuliko hii, Abu Daawuud na at-Tirmidhiy aliyesema:

“Hadiyth ni nzuri, Swahiyh na geni.”

Imepokelewa vilevile na Ibn Hibbaan na kwenye matamshi ya ´Abdur-Razzaaq imekuja:

“Walikuwa wakichinja ng´ombe au kitu kingine kwenye kaburi.”

´Aqr kwenye kaburi ni kuchinja karibu na makaburi. Kitendo hichi kilikuwa kinafanywa na washirikina kabla ya kuja Uislamu. Ni kitendo cha haramu katika Ummah huu. al-Khattwaabiy amefafanua maana ya maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) “Hakuna ´Aqr katika Uislamu” na kusema:

“Washirikina kabla ya kuja Uislamu walikuwa wakichinja ngamia kwenye makaburi. Anapokufa mtu sharifu au mkarimu, wanachinja kwenye kaburi lake. Walikuwa wakisema kuwa yeye mwenyewe alikuwa akiwachinjia wageni wake na hivi sasa na yeye afanyiwe. Kuna watu walikuwa wakisema ya kwamba walikuwa wakichinja ngamia kwenye makaburi kwa ajili ya kuwalisha wanyamapori na ndege ili kusemwe kuwa yule maiti ametoa chakula alipokuwa hai na baada ya kufa kwake. Imesemekana vilevile kuwa walikuwa wakiamini kuwa kiu cha yule maiti kinazimwa kwa kile chakula. Uislamu ukaja kukataza hayo.”

Bid´ah hii chafu inapatikana takriban katika kila kijiji pindi mtu anapokufa. Pindi mtu anapokufa katika mji watu wa mji wanakuja kwa ajili ya kutoa. Wanawachinjia kutoka katika ile mali ya maiti ambayo ni mirathi inayokwenda kwa warithi katika mayatima na wengineo. Haya nimeyashahudia mwenyewe na kuyasikia. Tunamuomba Allaah afanye kupatikane watawala wataiotokomeza Bid´ah hii.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 111-112
  • Imechapishwa: 21/10/2016