Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:
“Pepo na Moto vimeumbwa. Vimeshaumbwa, kama ilivyopokelewa kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyesema:
“Nimeingia Pepo na nimeona kasiri.”[1]
“Nimeona Kawthar.”[2]
“Nimetazama Pepo na kuona wakazi wake wengi ni… Nimetazama Moto na kuona wakazi wake wengi ni… “
Mwenye kudai kuwa havijaumbwa anaikadhibisha Qur-aan na Hadiyth za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Siamini kuwa mtu kama huyo anaamini Pepo na Moto.”
MAELEZO
Pepo na Moto vimeshaumbwa. Vimeumbwa kabla ya kuumbwa viumbe wengine. al-Bukhaariy katika “as-Swahiyh” kuhusu fadhilah za ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) na kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:
“Jana jioni niliingia Peponi nikaona kasiri ya dhahabu. Pambizoni na Pepo hiyo alikuwepo mwanamke akitawadha. Nikasema: “Ni kasiri ya nani hii?” Wakasema: “Ni ya mwarabu.” Nikasema: “Mimi ni mwarabu.” Nikasema: “Ni kasiri ya nani hii?” Wakasema: “Ni ya m-Quraysh.” Nikasema: “Mimi ni m-Quraysh.” Nikasema: “Ni kasiri ya nani hii?” Wakasema: “Ni ya ´Umar bin al-Khattwaab.” Nikataka kuingia ndani na kutazama, lakini nikakumbuka wivu wako, ee ´Umar, ndipo nikageuza na kuondoka zangu.” Ndipo ´Umar bin al-Khattwaab akaanza kulia na akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Hivi kweli nikuonee wivu wewe?”[3]
Dalili nyingine ni ile iliyotajwa kuhusiana na swalah ya kupatwa kwa jua. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:
“Nilionyeshwa Pepo upande wa ukuta huu mpaka nikatamani kuchukua moja ya vipande vyake. Lau ningechukua basi mgekila mpaka siku ya Qiyaamah. Nilionyeshwa Moto ambapo nikamuona ´Amr bin Luhayy akivuta matumbo yake. Nilimuona mwanamke mrefu kutoka katika Himyar akiparuliwa makucha na paka. Nikasema: “Ana nini mwanamke huyu?” Wakasema: “Alimfunga na hakumpa chakula wala kinywaji na wala hakumwacha huru akaenda kula katika wadudu wa ardhini.”[4]
Kuna dalili nyingi juu ya hili.
Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:
“Nimeona al-Khawthar.””
Haya yamepokelewa wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipoona al-Kawthar katika safari ya usiku. Aliweka mikono yake ndani yake na akaona namna udongo wake ulikuwa na harufu yenye nguvu ya miski.”
Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:
“Nimetazama Pepo na kuona wakazi wake wengi ni… Nimetazama Moto na kuona wakazi wake wengi ni… “
Kama ilivyokuja katika Hadiyth:
“Nimetazama Pepo na kuona wakazi wake wengi ni mafukara na nimetazama Moto na kuona wakazi wake wengi ni wanawake.”[5]
Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:
“Mwenye kudai kuwa havijaumbwa anaikadhibisha Qur-aan na Hadiyth za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Siamini kuwa mtu kama huyo anaamini Pepo na Moto.”
Kwa sababu atakuwa ni mwenye kumkadhibisha Allaah katika maelezo yake na ni mwenye kumkadhibisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika maelezo yake. Allaah (Ta´ala) amesema:
وَلَقَدْ رَآهُ نَزْلَةً أُخْرَىٰ عِندَ سِدْرَةِ الْمُنتَهَىٰ عِندَهَا جَنَّةُ الْمَأْوَىٰ
“Hakika amemuona katika uteremko mwingine katika mkunazi wa mpaka wa mwisho kabisa karibu yake kuna al-Jannah al-Ma´waa.”[6]
[1] al-Bukhaariy (3679).
[2] al-Bukhaariy (4964), Muslim (400) na Abu Ya´laa (3186).
[3] al-Bukhaariy (3679) na Muslim (2395).
[4] Muslim (904).
[5] al-Bukhaariy (3241) na Muslim (2737).
[6] 53:13-15
- Muhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
- Tarjama: Firqatunnajia.com
- Marejeo: Itmaam-ul-Minnah, uk. 166-170
- Imechapishwa: 06/06/2019
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window)
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window)
- Click to print (Opens in new window)
- Click to email a link to a friend (Opens in new window)
- Click to share on Facebook (Opens in new window)
- Click to share on Twitter (Opens in new window)
- Click to share on Pocket (Opens in new window)