50. Mlango kuhusu maneno Yake (Ta´ala) “Lakini anapowapa [mtoto mzima na] mwema [waliyemuomba], wanamfanyia washirika katika kile alichowapa! Ametukuka Allaah kutokana na yale yote wanayoshirikisha!”

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

فَلَمَّا آتَاهُمَا صَالِحاً جَعَلاَ لَهُ شُرَكَاء فِيمَا آتَاهُمَا فَتَعَالَى اللّهُ عَمَّا يُشْرِكُونَ

”Lakini anapowapa [mtoto mzima na] mwema [waliyemuomba], wanamfanyia washirika katika kile alichowapa! Ametukuka Allaah kutokana na yale yote wanayoshirikisha!” (al-A´raaf 07:190)

Ibn Hazm amesema:

“Wamekubaliana juu ya kuharamisha kila jina ambalo yule mwenye kuitwa hivyo ni mja wa mwingine badala ya Allaah. Kama mfano wa “´Abd-´Umar” na “´Abd al-Ka´bah”. “´Abdul-Muttwalib” limevuliwa katika hayo.”

2- Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema kuhusiana na Aayah hapo juu:

“Aadam alipomwendea mkewe alishika ujauzito. Ndipo Ibliys akawajia na kuwaambia: “Mimi ndiye yule niliyesababisha mkatolewa Peponi. Ima nitiini au vinginevyo nitamfanya mtoto wenu aote pembe mbili kama swala tumboni mwa mama yake ambazo zitapasua tumbo lake wakati wa kumzaa na ntafanya hivyo ntafanya hivyo.” Alisema hivo kwa ajili ya kuwatia khofu na akawaambia: “Mwiteni “´Abdul-Haarith”.” Wakakataa kumtii na mtoto akazaliwa hali ya kuwa ameshakufa. Kisha akabeba ujauzito mwingine ambapo akawajia kwa mara nyingine na akawaambia kama alivyowaambia mara ya kwanza ambapo akawakuta ni wenye kumpenda mtoto huyo kwelikweli na wakamwita jina la “´Abdul-Haarith”. Hiyo ndio tafsiri ya maneno Yake (Ta´ala):

فَلَمَّا آتَاهُمَا صَالِحاً جَعَلاَ لَهُ شُرَكَاء فِيمَا آتَاهُمَا فَتَعَالَى اللّهُ عَمَّا يُشْرِكُونَ

”Lakini anapowapa [mtoto mzima na] mwema [waliyemuomba], wanamfanyia washirika katika kile alichowapa! Ametukuka Allaah kutokana na yale yote wanayoshirikisha!”[1]

Ameipokea Ibn Abiy Haatim.

3- Naye (Ibn Haatim) ameipokea kwa cheni ya wapokezi Swahiyh kutoka kwa Qataadah aliyesema:

“Washirika inahusiana na kumshirikisha Allaah katika utiifu na si katika kumwabudu.”

4- Naye (Ibn Haatim) amepokea kwa cheni ya wapokezi Swahiyh kutoka kwa Mujaahid aliyesema kuhusiana na maneno Yake:

لَئِنْ آتَيْتَنَا صَالِحاً لَّنَكُونَنَّ مِنَ الشَّاكِرِينَ

”Ukitupa [mtoto mzima na] mwema basi kwa hakika tutakuwa katika wenye kushukuru.” (al-A´raaf 07:189)

Akasema:

“Walichelea mtoto asijekuwa si mtu.”

Maana kama hiyo imethibiti pia kwa al-Hasan, Sa´iyd na wengineo.

MAELEZO

Alichokusudia mwandishi kwa kichwa cha khabari hichi ni kwamba majina yenye kuashiria mtu ni mja wa mwingine asiyekuwa Allaah ni haramu. Kwa mfano haijuzu kwa mtu akaitwa ´Abdun-Nabiy, ´Abdul-Ka´bah au ´Abdul-Husayn. Majina yanayojuzu ni yale yenye kuashiria kuwa mtu ni mja wa Allaah pekee kama mfano wa ´Abdur-Rahmaan na ´Abdullaah. Kwa sababu Allaah amemsema vibaya yule mwenye kufanya hivo na akasema:

فَلَمَّا آتَاهُمَا صَالِحاً جَعَلاَ لَهُ شُرَكَاء فِيمَا آتَاهُمَا فَتَعَالَى اللّهُ عَمَّا يُشْرِكُونَ

”Lakini anapowapa [mtoto mzima na] mwema [waliyemuomba], wanamfanyia washirika katika kile alichowapa! Ametukuka Allaah kutokana na yale yote wanayoshirikisha!”

Hapa anasemwa vibaya na anakejeliwa yule mwenye kuitwa hivo. Mtiririko wa Aayah unamzungumzia Aadam na Hawwaa´ ambao walimtii shaytwaan na wakamwita mtoto wao jina la “´Abdul-Haarith”. Wako wengine waliosema kwamba Aayah inawazungumzia kundi la wana wa israaiyl. Lakini hata hivyo mtiririko wa Aayah unayakataa hayo. Bali ukweli wa mambo ni kama alivosema Ibn ´Abbaas na wengine katika Salaf. Wakatumbukia katika maasi. Mitume wanaweza kutumbukia katika maasi madogo, ndivo wasemavyo wanachuoni. Inawezekana vilevile kwamba pindi walipofanya hivo walikuwa wakidhani kuwa ni kitendo kinachofaa. Hawakujua kuwa ni kitendo cha madhambi. Kwanza walilichukia jambo hilo kisha baadaye wakategwa na wasiwasiwa wake. Miongoni mwa yale Allaah aliyomteremshia Mtume Wake akambainishia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba kitendo hicho hakijuzu. Hukumu ni yenye kufungamana na Shari´ah ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) iliyoenea. Shari´ah zilizotangulia ziko na mambo ambayo yanafaa na ziko na mambo yasiyofaa.

Ibn Hazm amesema:

“Wamekubaliana juu ya kuharamisha kila jina ambalo yule mwenye kuitwa hivyo ni mja wa mwingine badala ya Allaah. Kama mfano wa “´Abd-´Umar” na “´Abd al-Ka´bah”. “´Abdul-Muttwalib” limevuliwa katika hayo.”

Sababu ya kuvuliwa jina hili ni kwa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alilikubali na hakulibadilisha. Yupo Swahabah mwingine akiitwa ´Abdul-Muttwalib bin Rabiy´ah. Hili ni kwa sababu msingi wa jina hilo ni utumwa kwa mwanadamu. Walikuwa wakimwita Shaybah bin Hishaam “´Abdul-Muttwalib” kwa kuwa wakidhani kuwa ni mtumwa wa al-Muttwalib pindi wanapoona uso wake unapiga weusi baada ya safari. Ukweli wa mambo ni kwamba al-Muttwalib alikuwa ami yake. Jina hilo linakubalika katika Uislamu kinyume na majina mengine yote mfano wake.

3- Naye (Ibn Haatim) ameipokea kwa cheni ya wapokezi Swahiyh kutoka kwa Qataadah aliyesema:

“Washirika inahusiana na kumshirikisha Allaah katika utiifu na si katika kumwabudu.”

Kwa sababu walimtii juu ya jina hili pasi na wao kujua. Yote haya ni kwa minajili ya kuikamilisha Tawhiyd na kunyenyekea mbele ya Allaah na kufunga njia zote zinazopelekea katika shirki.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mimi ni mwana wa ´Abdul-Muttwalib.”

Huku ni kuelezea jina lililotangulia. Ni jambo halidhuru kwa sababu alikuwa akitambulika kwa jina hilo. Kadhalika inahusiana na majina kama “´Abdu Manaaf” na “´Abdu ´Amr” ikiwa yatatajwa kwa njia ya kuelezea.

[1] Ahmad (20129) na at-Tirmidhiy (3077). Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Dhwa´iyf-ul-Jaami´” (4769).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 148-150
  • Imechapishwa: 06/11/2018