49. Kumswalia mtoto na kipomoko swalah ya jeneza

Mlango huu ni mkubwa kwa kuwa ndani yake mna bishara kubwa kwa kila ambaye amempoteza mtoto wake. Kwa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametuamrisha kuwaswalia swalah ya jeneza watoto na kuwaombea du´aa wazazi wao.

Wanachuoni wengi wanasema kuwa watoto wachanga wanatakiwa kuswaliwa swalah ya jeneza kukiwemo kipomoko ilimradi kimeshapuliziwa roho. Baadhi ya Salaf wanaonelea kuwa mtoto mdogo haswaliwi midhali hajabaleghe. Nitabainisha udhaifu wa maoni haya.

al-Bukhaariy amepokea kuwa Ibn Shihaab amesema:

“Kila mtoto anayekufa anatakiwa kuswaliwa hata kama atakuwa ni mtoto wa nje ya ndoa. Kwa sababu mtoto huyo amezaliwa juu ya maumbile ya Uislamu na wazazi wake wanajinasibisha na Uislamu au angalau baba yake [anajinasibisha na Uislamu]. Haijalishi kitu hata kama mama yake sio muislamu. Mtoto akifa baada ya kupiga ukelele/kulia, anatakiwa kuswaliwa. Hata hivyo yule mtoto asiyepiga ukelele hatakiwi kuswaliwa, kwa kuwa ni mimba iliyoporomoka. Abu Hurayrah amepokea kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyesema: “Hakuna mtoto yeyote isipokuwa huzaliwa juu ya maumbile.”

Abu Daawuud amepokea kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliyesema:

“Ibraahiym, mtoto wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), alikufa akiwa na miezi 18 na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakumswalia.”

Katika mlolongo wa wapokezi kuna Muhammad bin Ishaaq na maneno ya wanachuoni juu yake yanajulikana. Hadiyth inasapotiwa na baadhi ya Salaf waliyosema kuwa mtoto haswaliwi swalah ya jeneza, lakini usahihi wa Hadiyth umetiwa dosari. Kumeshatangulia ya kwamba Ahmad amepokea kupitia kwa al-Baraa´ bin ´Aazib (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimswalia Ibraahiym. Ahmad amepokea kupitia kwa al-Mughiyrah bin Shu´bah kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyesema:

“Wapandaji wanatakiwa kuwa nyuma ya jeneza. Watembeaji wanatakiwa kuwa mbele kidogo upande wake wa kulia au wa kushoto. Kipomoko kinatakiwa kuombewa du´aa na wazazi wake waombewe msamaha na rehema.”

Ameipokea Abu Daawuud, an-Nasaa´iy na at-Tirmidhiy aliyesema:

“Hadiyth ni nzuri na Swahiyh.”

Ibn Maajah amepokea kwa matamshi:

“Wapandaji wanatakiwa kuwa nyuma ya jeneza. Watembeaji wanatakiwa kuwa mbele kidogo upande wake wa kulia au wa kushoto. Mtoto anatakiwa kuombewa du´aa na wazazi wake waombewe msamaha na rehema.”

Ibn Maajah badala ya “kipomoko” yeye ametaja mtoto.

Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mtoto haswaliwi na harithiwi na wala harithi mpaka apige ukelele/kulia wakati wa kuzaliwa.”

Ameipokea at-Tirmidhiy kupitia kwa Ismaa´iyl bin Muslim al-Makkiy. at-Tirmidhiy amesema:

“Hadityth hii imepokelewa kwa njia mbalimbali. Baadhi wameipokea kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wengine wameipokea kutoka kwa Swahabah. Kuwa ni maneno ya Swahabah ni sahihi zaidi kuliko maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Haafidhw adh-Dhwiyaa´ amesema:

“Wanachuoni wengi wamemzungumzia Ismaa´iyl bin Muslim al-Makkiy.”

Ibn Maajah amepokea kupitia kwa Jaabir aliyesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mtoto akipiga ukelele wakati wa kuzaliwa aswaliwe na kurithiwa.”

Katika mlolongo wa wapokezi kuna ar-Rabiy´ bin Yaziyd ambaye ni dhaifu. Amedhoofishwa na wanachuoni wengi. Haafidhw adh-Dhwiyaa´ amesema:

“Mtoto anatakiwa kuswaliwa midhali ameshapuliziwa roho pasi na kujali ikiwa atapiga ukelele wakati wa kuzaliwa au hatopiga.”

Huu ndio udhahiri wa maoni ya madhehebu ya Imaam Ahmad, mtoto ambaye kishapuliziwa roho aswaliwe swalah ya jeneza sawa ikiwa atapiga ukelele au hatopiga. Mtoto anapuliziwa roho anapotimiza miezi mine. Majd-ud-Diyn bin Taymiyyah amesema:

“Kipomoko hakiswaliwi swalah ya jeneza kabla ya kufikisha miezi mine. Hapa kitakuwa sio maiti kwa kuwa hakijapuliziwa roho.”

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

“Kukiswalia kipomoko ambacho hakijapuliziwa roho kumejengwa juu ya ufufuliwaji. Wanachuoni wana maoni mawili. Tukisema kuwa kitafufuliwa, kitaswaliwa, na tukisema kuwa hakitofufuliwa hakitoswaliwa – na Allaah ndiye anajua zaidi.”

Ahmad bin Abiy ´Abdah amesema:

“Nilimuuliza Abu ´Abdillaah Ahmad bin Hanbal: “Ni lini kipomoko kinaswaliwa swalah ya jeneza?” Akasema: “Pale kinapotimiza miezi mine. Kwa kuwa hapo kinakuwa kimeshapuliziwa roho.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 104-105
  • Imechapishwa: 19/10/2016