Ama jibu la kijumla

Kwa hakika ni jambo kubwa na faida kubwa kwa yule mwenye kulifahamu. Nalo ni Kauli Yake (Ta´ala):

هُوَ الَّذِي أَنزَلَ عَلَيْكَ الْكِتَابَ مِنْهُ آيَاتٌ مُّحْكَمَاتٌ هُنَّ أُمُّ الْكِتَابِ وَأُخَرُ مُتَشَابِهَاتٌ ۖ فَأَمَّا الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِمْ زَيْغٌ فَيَتَّبِعُونَ مَا تَشَابَهَ مِنْهُ ابْتِغَاءَ الْفِتْنَةِ وَابْتِغَاءَ تَأْوِيلِهِ ۗ وَمَا يَعْلَمُ تَأْوِيلَهُ إِلَّا اللَّـهُ

”Yeye ndiye Aliyeteremsha kwako Kitabu humo mna Aayah zilizo wazi – hizo ndio msingi wa Kitabu – na nyinginezo haziko wazi maana yake. Ama wale ambao katika nyoyo zao mna upotovu, hufuata zile zisizokuwa wazi kwa ajili ya kutafuta fitnah na kutafuta kupotosha [kwa kufasiri maana yake iliyojificha]; na hakuna ajuae tafsiri yake [iliyojificha] isipokuwa Allaah.” (Aal ´Imraan 03 : 07)

MAELEZO

Hili ni jibu la kijumla juu ya utata. Amesema (Ta´ala):

هُوَ الَّذِي أَنزَلَ عَلَيْكَ الْكِتَابَ

”Yeye ndiye Aliyeteremsha kwako Kitabu… “

Bi maana Qur-aan.

مِنْهُ آيَاتٌ مُّحْكَمَاتٌ هُنَّ أُمُّ الْكِتَابِ

“… humo mna Aayah zilizo wazi – hizo ndio msingi wa Kitabu…. “

Muhkam ni ile isiyohitajia nyingine katika ubainifu wake. Katika Qur-aan kuna Aayah ambazo ni Muhkamaat. Ni zile ambazo ziko wazi katika maana yake na hazihitajii zengine.

Hizo ndio msingi wa kitabu – Mama wa kitabu ni ule msingi unaorudiliwa. Aayah Muhkamaat ni zile za msingi ambazo zinarejelewa.

Nyinginezo haziko wazi maana yake – Mutashaabihah ni ile ambayo inaihitajia nyingine katika kubainisha maana yake. Katika hali hii inatakiwa kurudi katika ile ambayo ni Muhkam. Mutashaabihah inakuwa na uwezekano wa maana mbalimbali na hivyo inakuwa ni yenye kuhitajia nyingine katika kubainisha makusudio yake. Miongoni mwake kunaingia Aayah iliyoachiwa na iliyofutwa. Ametaja (Ta´ala) ilivyogawanyika misimamo ya watu juu ya Aayah ya Muhkam na Mutashaabihah. Amesema:

فَأَمَّا الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِمْ زَيْغٌ فَيَتَّبِعُونَ مَا تَشَابَهَ مِنْهُ

“Ama wale ambao katika nyoyo zao mna upotovu, hufuata zile zisizokuwa wazi… “

Wanachukua zile Aayah zisizokuwa wazi au zile Aayah zinazoweza kuwa na maana nyingi na kutumia kama dalili juu ya yale wanayoyataka pamoja na kuwa uwezekano wake sio dalili juu ya yale wanayoyasema. Wanachotaka ni kuwapaka watu mchanga wa machoni pindi wanapowaambia kuwa wanatumia dalili kwa Qur-aan. Matokeo yake wanachukua Aayah ambazo kwa dhati yake haziko wazi maana yake au Aayah zinazoweza kuwa na maana nyingi na hivyo wanatumia dalili juu ya yale wanayoyataka.

Kwa ajili ya kutafuta fitina… Bi maana kutatiza au kupotoa.

… au kutafuta kupotosha – Ta´wiyl inatumiwa katika maana mbili, kama alivyosema Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) katika kitabu chake “Tadmuriyyah”[1]:

Maana ya kwanza: Makusudio yake ni tafsiri. Hili ndilo lenye kujulikana kwa wale waliotangulia. Kwa ajili hiyo utamuona Ibn Jariyr at-Twabariy katika kitabu chake cha Tafsiyr ya Qur-aan akisema: “Maneno ya Ta´wiyl yake” akiwa na maana “Maneno ya tafsiri yake”. Ikiwa haya ndio yaliyokusudiwa katika Aayah:

وَمَا يَعْلَمُ تَأْوِيلَهُ إِلَّا اللَّـهُ

“… na hakuna ajuae Ta´wiyl yake isipokuwa Allaah.”

basi wale waliobobea katika elimu itaonganishwa namna hii:

وَمَا يَعْلَمُ تَأْوِيلَهُ إِلَّا اللَّـهُ ۗ وَالرَّاسِخُونَ فِي الْعِلْمِ

“… hakuna ajuae maana zake isipokuwa Allaah. Na wenye msingi madhubuti katika elimu… “(03:07)

Hapo italeta maana ya kwamba na wale waliobobea katika elimu pia wanajua tafsiri yake. Hilo ni kwa kuwa imerudishwa katika Muhkam inayobainisha malengo yake. Kuifasiri Qur-aan kwa sura kama hii hakuna ajuae isipokuwa Allaah na wanachuoni waliobobea. Kuhusu wasiokuwa wasomi na wajinga wao hawajui tafsiri yake. Wapindaji wanachukua Mutashaabihah yake na hawairudishi katika Muhkam. Mfumo wao ni kukata sehemu ya Qur-aan kutokamana na sehemu nyingine. Wanachukua baadhi ya Aayah na kuacha Aayah nyenginezo.

Maana ya pili: Maana ya pili ya Ta´wiyl ni uhakika wa jambo linavyoisha na hatima yake katika mustakabali. Mfano wa uhakika wa zabibu, mitende, matunda, maziwa, mvinyo, asali na vinginevyo vilivyomo Peponi. Hakuna ajuae uhakika wa vitu hivi isipokuwua Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala), kwa kuwa ni elimu iliyofichikana. Vilevile namna ya majina na sifa za Allaah hakuna anayejua uhakika wake isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Ta´wiyl kwa maana hii ni hatima ya kitu kitavyokuwa katika mustakabali. Ikiwa kimekusudiwa maana hii basi inatakiwa kuisoma Aayah na kuishia kwenye:

وَمَا يَعْلَمُ تَأْوِيلَهُ إِلَّا اللَّـهُ

“… na hakuna ajuae Ta´wiyl yake isipokuwa Allaah.”

Kwa sababu katika sura kama hii itakuwa hakuna anayejua uhakika wake, Ta´wiyl isipokuwa Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala).

[1] Uk. 809.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 67-68
  • Imechapishwa: 27/12/2016