48. Daraja za dini ni: Uislamu, Imani na Ihsaan

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Hili lina daraja tatu: Uislamu, Imani na Ihsaan. Kila daraja ina nguzo zake.

Nguzo za Uislamu ni tano: Kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan na kuhiji Nyumba ya Allaah takatifu.

MAELEZO

Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) amebainisha kwamba dini ya Kiislamu ina ngazi tatu na baadhi yazo ziko juu kuliko zengine. Ngazi hizo ni Uislamu, Imani na Ihsaan.

Dalili ya hilo ipo katika maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Hadiyth ambayo imepokelewa na kiongozi wa waumini ambaye ni ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) wakati Jibriyl alipokuja na kumuuliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu Uislamu, Imani na Ihsaan. Akabainisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hayo na kusema:

“Ilikuwa ni Jibriyl ambaye amewajia ili kuwafunza dini yenu.”

Nguzo za Uislamu ni tano – Dalili ya hilo ni Hadiyth ya Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) katika Hadiyth ambapo ameeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Uislamu umejengwa kwa matano: Kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan na kuhiji Nyumba ya Allaah takatifu.”[1]

[1] al-Bukhaariy (08), Muslim (16), at-Tirmidhiy (2736), an-Nasaaiy (5016), Ahmad (2/120) na al-Bayhaqiy (7322) kutoka kwa Ibn ´Umar.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 68-69
  • Imechapishwa: 28/05/2020