48. Ada imerudia akiwa katika Twawaaf-ul-Ifaadhwah

Swali 48: Kuna mwanamke alisafiri kwenda hajj na akajiliwa na ada ya mwezi kwa muda wa siku tano tangu ile tarehe ya safari yake. Alipofika katika kituo akaoga na akafunga Ihraam ilihali bado hajatwahirika kutokamana na ada yake. Wakati alipofika Makkah alikaa kivuli nje ya msikiti Mtakatifu na hakufanya chochote katika zile nembo za Hajj au ´Umrah. Akakaa siku mbili Minaa kisha akatwahirika ambapo akaoga na akatekeleza taratibu zote za ´Umrah akiwa ni msafi. Kisha damu ikamrudilia akiwa katika Twawaaf-ul-Ifaadhwah kwa ajili ya hajj. Isipokuwa tu aliendelea na akakamilisha taratibu za hajj na hakumweleza msimamizi wake isipokuwa baada ya kufika katika mji wake. Ni ipi hukumu ya hilo?

Jibu: Hukumu ni kwamba damu iliyompata katika Twawaaf-ul-Ifaadhwah ikiwa ni damu ya hedhi ambayo anaifahamu kwa maumbile na maumivu yake, basi Twawaaf-ul-Ifaadhwah haikusihi. Hivyo itamlazimu kurudi Makkah ili apate kutufu Twawaaf-ul-Ifaadhwah. Kwa hivyo ataingia katika ´Ihraam akiwa ni mwenye kufanya ´Umrah kuanzia hapo kituoni na afanye ´Umrah ikiwa na Twawaaf, Say´ na kufupisha kisha ndio afanye Twawaaf-ul-Ifaadhwah. Lakini damu hiyo ikiwa sio ya hedhi bali ni damu kimaumbile ya kawaida ambayo imetokamana na msongamano mkubwa, kutokwa na damu puani na mfano wa hayo, basi Twawaaf yake inasihi kwa wale ambao hawashurutishi twahara kwa ajili ya kutufu. Akiwa katika hali ya kwanza na mumewe asimwache kurudi kwa njia ya kwamba pengine anaishi katika nchi ya mbali basi hajj yake ni sahihi kwa sababu hawezi zaidi ya alichofanya.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: 60 su-aal wa jawaab fiy Ahkaam-il-Haydhw, uk. 39-40
  • Imechapishwa: 30/08/2021