Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

42 – Yeye ndiye mwisho wa Manabii, kiongozi wa wenye kumcha Allaah, bwana wa Mitume na kipenzi wa Mola wa walimwengu.

MAELEZO

Hizi ni baadhi ya sifa za Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Yeye ndiye mwisho wa Manabii. Maana yake ni kwamba hakuna Nabii mwingine atayekuja baada yake. Yeye ndiye amekhitimisha utume, kwa maana nyingine ni kwamba hatoongezwa wala kupunguzwa. Allaah amekhitimisha ujumbe kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amesema (Ta´ala):

مَّا كَانَ مُحَمَّدٌ أَبَا أَحَدٍ مِّن رِّجَالِكُمْ وَلَـٰكِن رَّسُولَ اللَّـهِ وَخَاتَمَ النَّبِيِّينَ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمًا

“Hakuwa Muhammad baba wa yeyote miongoni mwa wanaume wenu, lakini ni Mtume wa Allaah na ni mwisho wa Manabii. Na Allaah daima kwa kila kitu ni Mjuzi.”[1]

Hakuhitajiki kuja Nabii mwingine baada yake. Kwa sababu Qur-aan na Sunnah vipo. Wanazuoni wanaofuata mwenendo wa kiungu wapo. Wanalingania kwa Allaah na wanawazindua watu. Kwa hivyo dini ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) itaendelea kubaki mpaka kusimama kwa Qiyaamah. Haiwezi kubadilishwa wala kufutwa. Allaah ameifanya kuwa salama katika kila zama na katika kila mahali. Kuhusu Shari´ah za Mitume wengine zinakuwa za muda ambapo Allaah anazifuta kwa Shari´ah nyingine inayokuja inayoendana na Ummah huo:

لِكُلٍّ جَعَلْنَا مِنكُمْ شِرْعَةً وَمِنْهَاجًا

“Kwa kila Ummah katika nyinyi Tumeujaalia Shari’ah na mfumo wake.”[2]

لِكُلِّ أَجَلٍ كِتَابٌ

“Kwa kila kipindi kina hukumu.”[3]

Bi maana kila kitabu kina muda wake. Dini ya Uislamu imekamilika na haihitaji Mtume yeyote baada ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wanazuoni ndio warithi wa Mitume.

[1] 33:40

[2] 5:48

[3] 13:38

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 60-61
  • Imechapishwa: 06/12/2022