46. Pozo kwa wazazi waliofiliwa na mtoto mmoja

Allaah (Ta´ala) amesema:

وَالَّذِينَ آمَنُوا وَاتَّبَعَتْهُمْ ذُرِّيَّتُهُم بِإِيمَانٍ أَلْحَقْنَا بِهِمْ ذُرِّيَّتَهُمْ وَمَا أَلَتْنَاهُم مِّنْ عَمَلِهِم مِّن شَيْءٍ ۚ كُلُّ امْرِئٍ بِمَا كَسَبَ رَهِينٌ

“Wale walioamini na dhuriya yao ikawafuata kwa imani Tutawakutanisha nao dhuriya yao na hatutawapunguzia katika matendo yao chochote. Kila mmoja ni mwenye jukumu juu ya matendo yake.” 52:21

al-Baghawiy ametaja katika tafsiri yake ya Qur-aan kupitia kwa Sa´iyd bin Jubayr kutoka kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah hukinyanyua kizazi cha muumini katika ngazi yake kwa ajili ya kumfurahisha nao hata kama hawakufikia matendo yake.”

Kisha akasoma:

وَالَّذِينَ آمَنُوا وَاتَّبَعَتْهُمْ ذُرِّيَّتُهُم بِإِيمَانٍ أَلْحَقْنَا بِهِمْ ذُرِّيَّتَهُمْ وَمَا أَلَتْنَاهُم مِّنْ عَمَلِهِم مِّن شَيْءٍ ۚ كُلُّ امْرِئٍ بِمَا كَسَبَ رَهِينٌ

“Wale walioamini na dhuriya yao ikawafuata kwa imani Tutawakutanisha nao dhuriya yao na hatutawapunguzia katika matendo yao chochote. Kila mmoja ni mwenye jukumu juu ya matendo yake.” 52:21

Katika Aayah na Hadiyth hii kuna liwazo kwa wazazi waliompoteza mtoto wao. Hivi ndio wanatakiwa wazazi kuwa. Wanatakiwa kuwa katika hali nzuri. Kwa sababu hata kama watoto walikuwa wakubwa wanakufa kama waislamu wenye kumpwekesha Allaah. Na kama walikuwa wadogo ni miongoni mwa wale ambao hawatakiwi kuwa na khofu wala kuhuzunika kwa kuwa wamekufa juu ya maumbile salama. Ni miongoni mwa wenye furaha. Wataingia Peponi bila ya matendo waliyotenda. Allaah atawaingiza Peponi kwa sababu ya huruma na kuwatunuku Kwake. Kwenye kaburi mtoto atakuwa chini ya ulinzi wa babu yake Ibraahiym (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kiongozi wa wapwekeshaji. Imethibiti katika “as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy kupitia kwa Samurah bin Jundub aliyesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kuhusu ndoto yake:

“Ama yule mwanaume mrefu kwenye bustani alikuwa ni Ibraahiym (´alayhis-Salaam) na wale watoto waliomzunguka wote walikuwa ni watoto waliokufa katika maumbile.” Kukasemwa: “Watoto wa washirikina pia?” Akasema: “Watoto wa washirikina pia.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Ama yule mwanaume mrefu kwenye bustani alikuwa ni Ibraahiym (´alayhis-Salaam) na wale watoto waliomzunguka walikuwa ni watoto wa watu.”

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna mtoto yeyote isipokuwa huzaliwa juu ya maumbile. Kisha wazazi wake ndio humfanya akawa myahudi, mnaswara au mwabudu moto.”

Kisha Abu Hurayrah akasema:

“Ukipenda soma:

فَأَقِمْ وَجْهَكَ لِلدِّينِ حَنِيفًا ۚ فِطْرَتَ اللَّـهِ الَّتِي فَطَرَ النَّاسَ عَلَيْهَا ۚ لَا تَبْدِيلَ لِخَلْقِ اللَّـهِ ۚ ذَٰلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ

“Basi [wewe mwenye kutafuta haki] uelekeze uso wako wote kwenye imani iliyosafi na ya asli, imani ambayo Allaah [wakati wa uumbaji] amewaumbia watu kwayo – hakuna mabadiliko katika uumbaji wa Allaah! Hii ndio imani ya milele ya kweli, lakini watu wengi hawajui [haya].” 30:30

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim na matamshi ni ya al-Bukhaariy.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 97-98
  • Imechapishwa: 15/10/2016