45. Khofu kwa mpwekeshaji ambaye si msomi dhidi ya wapotevu

Hata hivyo khofu iko kwa yule mpwekeshaji ambaye anapita katika njia bila ya kuwa na silaha.

MAELEZO

Huu ndio uhakika wa mambo. Mpwekeshaji ambaye anapita njia na kuwaelekeza makafiri na kusema kuwa analingania katika dini ya Allaah ilihali hana elimu, mtu kama huyu anaposimamiwa na mmoja katika wasiokuwa wasomi wao na akamtupia utata hatoweza kujibu. Haya ni miongoni mwa mambo yanayowawajibishia wanafunzi na khaswa wale wanaolingania kwa Allaah waielewe dini ya Allaah na wajifunze hoja na dalili za Allaah na waisome ile batili iliyoko kwa wapinzani, makafiri na wanafiki. Lengo ni ili aweze kuzitwanga vizuri na kuzitambua. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pindi alipomtuma Mu´aadh kwenda Yemen alimwambia:

“Hakika wewe unawaendea watu katika Ahl-ul-Kitaab.”[1]

Alimwambia hivi ili kumwandaa kwa kuwa mbele yake kuna Ahl-ul-Kitaab na wasomi ambao wana hoja, utata na utatizi. Ni lazima Mu´aadh (Radhiya Allaahu ´anh) ajiweke tayari ili aweze kusimama kidete kwa ajili ya kulingania katika dini ya Allaah na kuraddi batili. Halafu akasema:

“Hivyo basi, iwe jambo la kwanza utakalowalingania ni ´nashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah` na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah.”[2]

Haya yanazidi kutilia nguvu wale wapwekeshaji wote kwa jumla na khaswa wanafunzi na wanaokuja msitari wa mbele kabisa ni wale wanaolingania katika dini ya Allaah wajifunze yale ambayo kwayo wataweza kujitetea na batili na kwayo waweze kuinusuru haki. Vinginevyo wataanguka mbele ya kila utata wataoelekezewa. Tatizo linakuja kwa yule mlinganizi anayelingania katika dini ya Allaah akishindwa kuijibu shubuha aliyotatizwa nayo mbele ya watu au akajibu kwa ujinga. Hili ni baya zaidi. Haya hayapingani na yale aliyosema Shaykh:

“Mtu ambaye si msomi katika wapwekeshaji anashinda watu elfu katika wanachuoni wa washirikina hawa.”

Kwa kuwa mpwekeshaji ambaye si msomi – pamoja na kuwa hali yake ndo iko hivo – ni lazima kwake kuwa na khofu kutokamana na shari yao na achukue tahadhari kwa kujifunza elimu yenye manufaa.

[1] al-Bukhaariy (4090), Muslim (19), at-Tirmidhiy (625), an-Nasaa´iy (2435), Abu Daawuud (1584), Ibn Maajah (1783), Ahmad (01/233) na ad-Daarimiy (1614).

[2] Muslim (19), at-Tirmidhiy (625), an-Nasaa´iy (2435), Abu Daawuud (1584), Ibn Maajah (1783), Ahmad (01/233) na ad-Daarimiy (1614).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 62-64
  • Imechapishwa: 17/12/2016