Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya kuchinja ni maneno Yake (Ta´ala):

قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ لَا شَرِيكَ لَهُ ۖ وَبِذَٰلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ

“Sema: “Hakika swalah yangu, kichinjwa changu, uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah pekee, Mola wa walimwengu. Hana mshirika; na kwa hayo ndio nimeamrishwa, nami ni muislamu wa kwanza [kujisalimisha].” (al-An´aam 06 : 162-163)

na katika Sunnah:

“Allaah amemlaani yule mwenye kuchinja kwa ajili ya asiyekuwa Allaah.”[1]

MAELEZO

Kuchinja ni kule kuizima roho kwa kumwaga damu kwa njia maalum. Hili linakuwa kwa njia mbalimbali zifuatazo:

1- Kuchinja kwa ´ibaadah kwa njia ya kwamba mtu akakusudia kuadhimisha kile kinachochinjiwa, kujidhalilisha kwacho na kujikurubisha kwacho. Hili haliwi isipokuwa Allaah (Ta´ala) pekee, kwa njia ambayo imewekwa na Allaah (Ta´ala). Aina hii kumfanyia mwingine asiyekuwa Allaah inazingatiwa ni shirki kubwa. Dalili ya hilo ni yale aliyosema Shaykh (Rahimahu Allaah), nayo ni maneno Yake (Ta´ala):

قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ لَا شَرِيكَ لَهُ

“Sema: “Hakika swalah yangu, kichinjwa changu, uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah pekee, Mola wa walimwengu.” Hana mshirika.”

2- Mtu kuchinja katika mnasaba wa kumkirimu mgeni, karamu ya ndoa na mfano wa hayo. Hili limeamrishwa. Kitendo hicho mara kinaweza kuwa cha lazima au kilichopendekezwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule anayemwamini Allaah na siku ya Mwisho, basi amkirimu mgeni wake.”[2]

Alisema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf:

“Fanya walima ijapo mbuzi.”[3]

3- Mtu akachinja kwa ajili ya kujiburudisha, kwa ajili ya biashara na mfano wa hayo. Jambo hili ni katika vigawanyo vya kufaa. Kimsingi ni kwamba inafaa. Hilo ni kutokana na maneno Yake (Ta´ala):

أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّا خَلَقْنَا لَهُم مِّمَّا عَمِلَتْ أَيْدِينَا أَنْعَامًا فَهُمْ لَهَا مَالِكُونَ وَذَلَّلْنَاهَا لَهُمْ فَمِنْهَا رَكُوبُهُمْ وَمِنْهَا يَأْكُلُونَ

“Je, hawaoni kwamba Sisi tumewaumbia – kutokana na yale iliyofanya mikono Yetu – [tukawaumbia] wanyama wa mifugo, basi wao wanawamiliki na tumewadhalilisha kwao, basi baadhi yao humo wanawapanda na wengine humo wanawala?” (Yaa Siyn 36 : 71-72)

Aina hii inaweza kuwa yenye kutakikana au yenye kukatazwa, itategemea itatumiwa kwa kitu gani.

[1] Muslim (1978), Ahmad (1/108) na an-Nasaa´iy (4434).

[2] al-Bukhaariy (6019), Muslim (48), Ahmad (2/174), Ibn Maajah (3672), ad-Daarimiy (2035) na Maalik (4/22) na al-Qabas.

[3] al-Bukhaariy (3781), Muslim (1427), Ahmad (3/165), Abu Daawuud (2109), at-Tirmidhiy (1100), Ibn Maajah (1907), ad-Daarimiy (2204) na Maalik (3/85) na al-Qabas. Tazama ”Aadaab-iz-Zafaaf”, uk. 149 ya al-Albaaniy.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 66
  • Imechapishwa: 28/05/2020