Shaykh-ul-Islaam bin Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa salam):

“Hakuna yeyote katika nyinyi isipokuwa Mola Wake atamsemeza. Kutakuwa hakuna baina yake na Yake mwenye kutarjumu.”[1]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu Ruqyah ya mgonjwa:

“Yule ambaye atahisi maumivu mmoja wenmau, au akahisi maumivu ndugu yake, aseme: “Mola wetu ni Allaah ambaye yuko mbinguni. Limetakasika jina Lako. Amri Yako iko mbinguni na ardhini kama ambavyo huruma Yako iko mbinguni. Tusamehe madhambi na makosa yetu. Wewe ni Mola wa wazuri. Teremsha rehema Yako na dawa Yako kwa huyu anayehisi maumivu.” ili aweze kupona.”[2]

Ameipokea Abu Daawuud na wengineo.

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Je, hamniamini na mimi nimeaminiwa na Aliye juu ya mbingu?”[3]

“´Arshi iko juu ya maji na Allaah Yuko juu ya ´Arshi Naye Anajua yale mliyomo.”[4]

Hadiyth ni nzuri na ameipokea Abu Daawuud n wengineo.

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia kijakazi:

“Yuko wapi Allaah?” Akasema: “Mbinguni.” Kisha akamuuliza: “Mimi ni nani?” Akasema: “Wewe ni Mtume wa Allaah.” Akasema: “Mwache huru, kwani hakika ni muumini.”[5]

Ameipokea Muslim.

“Imani bora kabisa ni wewe kutambua kuwa Allaah yuko pamoja na wewe popote unapokuwa.”[6]

Hadiyth ni nzuri.

“Anaposimama mmoja wenu ndani ya swalah, basi asiteme mate mbele yake wala kuliani mwake, kwani hakika Allaah Yuko mbele Yake. Badala yake [ateme] kushotoni mwake au chini ya mguu wake.”[7]

MAELEZO

Hizi ni sehemu ya Hadiyth ambazo zimepokelewa kuhusu sifa. Baadhi ya sifa hizi zimekwishatangulia. Lengo la mtunzi (Rahimahu Allaah) ni kutaja sehemu katika Aayah na Hadiyth zilizothibiti kuhusu sifa ili muislamu apate kujua makusudio yake. Ametaja baadhi ya mifano ya Aayah na Hadiyth zilizopokelewa kuhusu majina na sifa za Allaah.  Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanaamini yale yaliyofahamishwa na majina na sifa hizo. Wanazipitisha kama zilivyokuja pasi na kuzipotosha, kuzikanusha, kuzifanyia namna na kuzilinganisha. Ahl-us-Sunnah hawazipingi kama wanavyofanya Jahmiyyah na Mu´tazilah. Hawazifasiri kwa kupindisha maana kama wanavyofanya baadhi ya Maaturiydiyyah, Ashaa´irah na wengineo. Wanazipitisha kama zilivyokuja. Sambamba na hilo wanaziamini, wanazithibitisha na wanaitakidi yale yenye kufahamishwa na majina na sifa hizo na wakati huohuo wanamtakasa Allaah kufanana na viumbe Wake. Kwa hiyo Ahl-us-Sunnah hawaonelei ukanushaji wala ufananizi. Ni Aayah na Hadiyth vilivyothibiti na maana yake ni sahihi. Ndani yake hamna ufananizi, ushabihishaji wala ukanushaji. Miongoni mwazo ni maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhiwa salam):

“Hakuna yeyote katika nyinyi isipokuwa Mola Wake atamsemeza. Kutakuwa hakuna baina yake na Yake mwenye kutarjumu.”

Bi maana mkati na kati.

Hii ni dalili yenye kuonyesha kuwa kuzungumzishwa itakuwa kwa watu wote siku ya Qiyaamah. Lakini hata hivyo waovu watazungumzishwa kwa maneno yenye kuwadhuru na ya kuwaghadhibikia. Upande mwingine wema watazungumzishwa kwa maneno yenye kuwafurahisha.

Vilevile amesema (´alayhis-Swalaatu was-Salaam):

“Je, hamniamini na mimi nimeaminiwa na Aliye juu ya mbingu?”

“Mola wetu ni Allaah ambaye yuko mbinguni.”

“Teremsha rehema Yako na dawa Yako kwa huyu anayehisi maumivu.”

Zote hizi zinajulisha ujuu.

Amesema tena (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“´Arshi iko juu ya maji na Allaah Yuko juu ya ´Arshi Naye Anajua yale mliyomo.”

Haya ni kama mfano wa yale yaliyotangulia katika maneno Yake (Ta´ala):

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

”Mwingi wa rehema amelingana juu ya ´Arshi.” (20:05)

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Anaposimama mmoja wenu ndani ya swalah, basi asiteme mate mbele yake wala kuliani mwake, kwani hakika Allaah Yuko mbele Yake. Badala yake [ateme] kushotoni mwake au chini ya mguu wake.”

Allaah yuko juu ya ´Arshi na wakati huohuo yuko mbele ya mswaliji. Hakuna kipingamizi. Hakika Allaah yuko pamoja nasi popote tunapokuwa. Amesema (Ta´ala):

وَهُوَ مَعَكُمْ أَيْنَ مَا كُنتُمْ وَاللَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ

“Naye yupamoja nanyi popote mlipo, na Allaah kwa myatendayo ni Mwenye kuyaona.” (57:04)

“Imani bora kabisa ni wewe kutambua kuwa Allaah yuko pamoja na wewe popote unapokuwa.”

Yeye yuko pamoja naye kwa ujuzi Wake na wakati huohuo yuko juu ya mbingu kwa dhati Yake (Jalla wa ´Alaa). Yuko juu na wakati huohuo yuko pamoja nasi kwa kutuzunguka kiujuzi (Jalla wa ´Alaa). Yeye (Subhaanah) yuko juu ya ´Arshi na juu ya viumbe wote na wakati huohuo ujuzi Wake uko kila mahali. Hakuna chochote asichokijua kutokana na ujuzi Wake (Jalla wa ´Alaa). Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema katika kisa cha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiwa pamoja na as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh) pindi (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliposema ilihali wamo pangano:

لَا تَحْزَنْ إِنَّ اللَّـهَ مَعَنَا

“Usihuzunike – hakika Allaah yupamoja nasi!” (09:40)

Vilevile amesema katika kisa cha Muusa na Haaruun (´alayhimaas-Swalaatu was-Salaam):

 لَا تَخَافَا ۖ إِنَّنِي مَعَكُمَا أَسْمَعُ وَأَرَىٰ

“Msikhofu! Hakika Mimi niko pamoja nanyi; nasikia na naona.” (20:46)

وَاصْبِرُوا ۚ إِنَّ اللَّـهَ مَعَ الصَّابِرِينَ

“Na subirini! Hakika Allaah yupamoja na wanaosubiri.” (08:46)

Huu ni upamaja wa kimaalum na wenye kuenea:

وَهُوَ مَعَكُمْ أَيْنَ مَا كُنتُمْ وَاللَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ

“Naye yupamoja nanyi popote mlipo, na Allaah kwa myatendayo ni Mwenye kuyaona.”

Ni wajibu kwa waislamu kutambua jambo hili ya kwamba Allaah yuko pamoja na viumbe Wake kwa kuwazunguka kiujuzi. Kadhalika kwamba yuko pamoja na mawalii Wake kiujuzi, kuwaangalia, kuwahifadhi na kuwajali (Subhaanahu wa Ta´ala) na wakati huohuo yuko juu ya ´Arshi (Subhaanahu wa Ta´ala) na juu ya viumbe wote. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ رَبَّكُمُ اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ

“Hakika Mola wenu ni Allaah Ambaye ameumba mbingu na ardhi katika siku sita, kisha akalingana juu ya ´Arshi.” (07:54)

Yeye (Jalla wa ´Alaa) yuko juu ya ´Arshi na ujuzi Wake umeenea kila mahali (Subhaanahu wa Ta´ala). Ni wajibu kwa kila muislamu ambaye ´ibaadah ni yenye kumuwajibikia kuitakidi ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ikiwa ni pamoja na kuamini kuwa Allaah yuko juu, kwamba amelingana juu ya ´Arshi, hakuna chochote kinachofichikana Kwake na ujuzi Wake umewazunguka waja Wake popote wanapokuwa.

[1] al-Bukhaariy (7443) na Muslim (1016)

[2] Abuu Daawuud (3892), an-Nasaa´iy (10876), al-Haakim (1/344) na (3/218) na wengine.

[3] al-Bukhaariy (3610, 3344, 4351 na 7433), Muslim (1064) na Abu Daawuud (4764).

[4] Muslim (537), Abu Daawuud (930), an-Nasaa’iy (3/13), Maalik (2/776), Ibn Abiy ´Aaswim (479), al-Bayhaqiy, uk. 422, Ahmad (5/447) na Abu Daawuud at-Twayaalisiy (1105).

[5] Muslim (537).

[6] at-Twabaraaniy katika ”al-Mu´jam al-Awsatw” (8791).

[7] al-Bukhaariy (406) na Muslim (547).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah, uk. 63-65
  • Imechapishwa: 24/10/2024