Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

Miongoni mwa mfumo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni kufuata mapokezi ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kwa undani na kwa uinje, na kufuata njia ya waliotangulia katika Wahajiri na Wanusuraji, na kufuata wasia wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pindi aliposema:

“Jilazimisheni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu wenye kuognoza baada yangu. Shikamaneni nazo barabara na ziumeni kwa magego yenu. Na tahadharini na mambo yaliyozuliwa, kwani hakika kila Bid´ah ni upotevu.”[1]

Wanatambua ya kwamba mazungumzo ya kweli kabisa ni maneno ya Allaah na uwongofu bora ni wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wanayapa kipaumbele maneno ya Allaah yatangulie mbele kabla ya maoni ya watu wengine na wanatanguliza uwongofu wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kabla ya uongofu wa wengine wote. Kwa ajili hii ndio maana wakaitwa watu wa Qur-aan na Sunnah. Ndio maana wanaitwa pia watu wa Mkusanyiko. Mkusanyiko kinyume chake ni mgawanyiko ingawa neno hilo limekuwa ni alama ya kundi la watu waliokusanyika.

Maafikiano ndio msingi wa tatu unaotegemewa katika elimu na dini. Kwa misingi hii mitatu wanayapima maneno na matendo yote ya watu yenye mahusiano na dini, ni mamoja ya ndani na ya nje. Maafikiano yanayodhibitiwa ni yale waliyoafikiana juu yake Salaf, kwa sababu baada yao kulikithiri tofauti na ummah ukagawanyika.

MAELEZO

Miongoni mwa misingi ya Ahl-us-Sunnah ni kufuata mapokezi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na yale waliyokuwemo makhaliyfah waongofu. Huu ni mwenendo wa Ahl-us-Sunnah. Wanafuata mfumo wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), mapokezi yake na mapokezi ya makhaliyfah wake waongofu. Hii ndio njia ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Kwa ajili hiyo wakaitwa watu wa Qur-aan na Sunnah. Wanaitwa pia watu wa Mkusanyiko. Mkusanyiko kinyume chake ni mgawanyiko ingawa neno hilo limekuwa ni alama ya kundi la watu waliokusanyika. Wameitwa pia Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah kwa sababu wamekusanyika juu ya Qur-aan na Sunnah, wakayasadikisha na wakayapima mambo yao kwavyo. Hawa ndio Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah kwa sababu wamekusanyika katika kuiadhimisha na kuitendea kazi Qur-aan na Sunnah. Kwa misingi hii mitatu wanayapima maneno na matendo yote ya watu yenye mahusiano na dini, ni mamoja ya ndani na ya nje.

Msingi wa kwanza ni Qur-aan. Msingi wa pili ni Sunnah. Msingi wa tatu ni maafikiano yenye kudhibitiwa. Inahusiana na yale maafikiano ya Salaf ambayo ni ya Maswahabah. Maneno na vitendo vyote vinavyofanywa na watu vinapimwa na misingi hii. Yanayoafikiana navyo yanakubaliwa na yanayoenda kinyume navyo anarudishiwa mwenye nayo. Pasi na kujali atakuwa ni nani.

[1] Abu Daawuud (4607), at-Tirmidhiy (2676) na Ibn Maajah (34). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”al-Irwaa’” (2455).

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah, uk. 121-122
  • Imechapishwa: 03/11/2024