Haafidhw Ibn Hajar al-´Asqalaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:
26 – Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:
“Mtumzima mzee amepewa ruhusa ya kutofunga. Badala yake atatakiwa kumpa chakula maskini kwa kila siku moja na halazimiki kulipa.”[1]
Ameipokea ad-Daaraqutwniy na al-Haakim. Wote wawili wameisahihisha.
MAELEZO
Masimulizi haya ni dalili kwamba mzee mkongwe ambaye hawezi kufunga ana ruhusa ya kula na kulisha chakula masikini kwa kila siku na hana ulazima wa kulipa kwa kufunga baadaye. Hukumu hiyohiyo inamuhusu mwanamke mzee asiyeweza kufunga na vilevile yule anayepata uzito katika swawm kama mgonjwa asiye na matumaini ya kupona, ambaye hawezi kufunga, basi huyu anahesabiwa kama mzee mkongwe; kwa sababu hataweza kulipa kwa kufunga muda wa kuwa ugonjwa wake ni wa kudumu. Maneno yake Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhuma) ndiyo yenye kutegemewa katika masuala haya. Dhahiri ni kwamba hakuna Swahabah aliyempinga na huenda alisikia kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa dalili ya maneno yake:
“Mtumzima amepewa ruhusa… “
Pia inawezekana amejitahidi kutokana na maneno Yake Allaah (´Azza wa Jall):
لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا
“Allaah hakalifishi nafsi yoyote isipokuwa kwa kadiri ya uwezo wake.”[2]
Na mfano wa Aayah kama hizo.
Ibn-ul-Mundhir na Ibn Hazm wamenukuu maafikiano juu ya hilo[3].
al-Bukhaariy amepokea kwa cheni yake kutoka kwa ´Atwaa´ kwamba alimsikia Ibn ´Abbaas akisoma:
وعلى الذين يطوقونه فدية طعام مسكين
”Na ni juu ya wale wanaoiweza [kufunga swawm] lakini kwa kujikalifisha[4] watoe fidia kulisha masikini.”
Ibn ´Abbaas amesema:
“Haijafutwa. Hiyo inamuhusu mzee mkongwe na mwanamke mzee wasioweza kufunga, basi watalisha masikini badala ya kila siku moja.”[5]
Haya ni maoni ya Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa), kwamba Aayah haijafutwa. Bali imebaki kuwa hukumu thabiti kwa wale wanaopata mashaka katika swawm kama wazee na wagonjwa wa kudumu, kama ilivyonukuliwa kutoka kwake katika riwaya nyingine. Aidha imepokelewa kutoka kwake maneno yanayoashiria kwamba imefutwa kutokana na maneno ya Allaah:
فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ
“Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi [mpya] na afunge swawm.”[6]
ndio maoni ya wanazuoni wengi kwamba mwanzoni mwa faradhi ya swawm, mtu alikuwa na khiyari ya kula na kulisha masikini au kufunga, kisha hukumu hiyo ikafutwa. Hakuna mgongano katika yale yaliyopokelewa kutoka kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa); kwani kufutwa kwa hukumu kunakanusha kuondolewa kabisa kwa hukumu, ilihali kufutwa kunakothibitishwa ni kuhusisha baadhi ya sehemu za hukumu ya jumla. Wanazuoni wa mwanzo walikuwa wakitumia neno ´kufutwa´ wakimaanisha kuhusisha baadhi ya hukumu, kama alivyotaja al-Qurtwubiy[7]. Kwa hivyo basi hukumu ya Aayah imefutwa kwa wale wanaoweza kufunga na imebaki kwa wale wasioweza isipokuwa kwa mashaka na tabu.
Mzee asiyeweza kufunga na wenye hukumu kama hiyo wana khiyari katika namna ya kutoa fidia: anaweza kuitoa kwa kuwagawia masikini nafaka, kiasi cha Mudd moja ya ngano kwa kila mmoja, ambacho kinakadiriwa kuwa takriban gramu 563 – kama ilivyotangulia katika zakaah – au anaweza kupika chakula na kuwaalika masikini kwa idadi ya siku alizokula, kama ilivyopokelewa kutoka kwa Anas (Radhiya Allaahu ´anh) kwamba alidhoofika kufunga mwaka mmoja, basi akatayarisha sahani kubwa ya Thariyd na kuwaalika masikini thelathini na akawashibisha[8] – na Allaah ndiye mjuzi zaidi.
[1] ad-Daaraqutwniy (2380) na al-Haakim (1/440).
[2] 02:286
[3] al-Ijmaa´, uk. 53 na ”Maraatib-ul-Ijmaa´”, uk. 47.
[4] Kwa maana wanaojikalifisha kufunga.
[5] Swahiyh-ul-Bukhaariy (4505).
[6] Ibn-ul-Jaaruud (381) na Ibn Jariyr (03/425).
[7] Tafsiyr al-Qurtwubiy (02/288).
[8] ad-Daaraqutwniy (02/207) na mlolongo wa wapokezi ni Swahiyh.
- Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
- Tarjama: Firqatunnajia.com
- Marejeo: Minhat-ul-´Allaam fiy Sharh Buluugh-il-Maraam (05/61-62)
- Imechapishwa: 26/02/2025
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window)
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window)
- Click to print (Opens in new window)
- Click to email a link to a friend (Opens in new window)
- Click to share on Facebook (Opens in new window)
- Click to share on Twitter (Opens in new window)
- Click to share on Pocket (Opens in new window)