43. Qur-aan inatakiwa kusomwa vizuri na kwa utaratibu

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akisoma Qur-aan kama alivyomwamrisha Allaah (Ta´ala); sio mbiombio wala polepole. Akitamka kila herufi kwa wazi kabisa[1]. Alikuwa anaweza kuirefusha Suurah mpaka inakuwa ndefu kuliko ilivyo[2].

Amesema:

“Kutasemwa kuambiwa msomaji wa Qur-aan: “Soma, upande na usome taratibu na kwa uzuri kama ulivyokuwa ukisoma duniani. Hakika ngazi yako itakuwa ile Aayah ya mwisho utayosoma.”[3]

Akirefusha kisomo chake kama mfano wa:

بِسْمِ اللّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ

“Kwa jina la Allaah, Mwingi wa huruma, Mwenye kurehemu.”[4]

na:

وَالنَّخْلَ بَاسِقَاتٍ لَّهَا طَلْعٌ نَّضِيدٌ

“… na mitende mirefu yenye makole yaliyozaa [tende] kwa wingi.”[5][6]

Alikuwa akisimama katika kila Aayah kama tulivyotangulia kubainisha.

Ilikuwa ikitokea wakati mwingine akivutia sauti yake[7]. Kwa mfano kama alivyofanya wakati wa kufunguliwa kwa Makkah pindi alipokuwa amekaa juu ya ngamia wake na akasoma Suurah “al-Fath” kisomo kilaini[8]. ´Abdullaah bin Mughaffal amesema kuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivutia namna hii:

“AaAaAa… “

Ameamrisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kupamba sauti wakati wa kusoma Qur-aan na kusema:

“Ipambeni Qur-aan kwa sauti zenu. Hakika sauti nzuri inaifanya Qur-aan kuzidi kuwa nzuri zaidi.”[9]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ambaye anasoma Qur-aan kwa sauti nzuri ni yule ambaye, pindi mnapomsikiliza akisoma, mnaona kuwa anamcha Allaah.”[10]

Ameamrisha kuiremba Qur-aan na kusema:

“Jifuzeni Kitabu cha Allaah, dumisheni kuisoma, ihifadhini na irembeni. Ninaapa kwa Yule ambaye nasfi yangu iko mikononi Mwake inakimbia haraka kuliko ngamia anavyochopoka kwenye kamba.”[11]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) vilevile:

“Si katika sisi yule asiyeiremba Qur-aan.”[12]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah hasikilizi kiti kama anavyomsikiliza Mtume mmoja kwa sauti ya kupendeza.”[13]

Alimwambia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Abu Muusa al-Ash´ariy (Radhiya Allaahu ´anh):

“Lau ungeniona namna ninavyosikia kisomo chake jana jioni. Umepewa moja katika sauti nzuri kabisa za Daawuud.” Abu Muusa akasema: “Ningelijua kama umesimama pale basi ningekusomea vizuri na kwa kuremba zaidi.”[14]

[1] Ibn-ul-Mubaarak katika ”az-Zuhd” (1/162), Abu Daawuud na Ahmad kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh.

[2] Muslim na Maalik.

[3] Abu Daawuud na at-Tirmidhiy ambaye ameisahihisha.

[4] al-Bukhaariy na Abu Daawuud.

[5] 50:10

[6] al-Bukhaariy katika ”Khalq Af´aal-il-´Ibaad” kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh.

[7] al-Munaawiy amesema:

”Mara nyingi ni kwamba inakuja kwa kuwa na hisia ya shangwe na furaha, ambayo mteuliwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa nayo kwa kuuteka mji wa Makkah.”

[8] al-Bukhaariy na Muslim.

[9] al-Bukhaariy kwa mlolongo wa wapokezi pungufu, Abu Daawuud, ad-Daarimiy, al-Haakim na Tammaam ar-Raaziy kwa isnadi mbili Swahiyh.

Uzinduzi

Baadhi ya wapokezi wameichanganya Hadiyth ya kwanza na kuipokea:

”Ipambeni Qur-aan kwa sauti zenu.”

Hili ni kosa katika upokezi na uelewa. Yule ambaye ameisahihisha basi amedidimia ndani ya kosa kwa kuwa inaenda kinyume na mapokezi na maelezo Swahiyh katika suala hili. Kosa hili ni mfano mzuri wa Hadiyth iliyopinduliwa juu na chini. Maelezo zaidi kuhusu ufupisho huu yanapatikana katika ”al-Ahaadiyth adh-Dhwa´iyfah” (5328).

[10] Swahiyh. Ibn-ul-Mubaarak katika ”az-Zuhd” (1/162), ad-Daarimiy, Ibn Naswr, at-Twabaraaniy, Abu Nu´aym katika ”Akhbaar Aswbahaan” na adh-Dhwiyaa’ katika ”al-Mukhtaarah”.

[11] ad-Daarimiy na Ahmad kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh.s

[12] Abu Daawuud na al-Haakim aliyeisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

[13] al-Bukhaariy, Muslim, at-Twahaawiy na Ibn Mandah katika ”at-Tawhiyd” (1/81).

[14] ´Abdur-Razzaaq katika ”al-Amaaliy” (1/44/2), al-Bukhaariy, Muslim, Ibn Naswr na al-Haakim.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 108-111
  • Imechapishwa: 17/02/2017