Mtunzi wa kitabu amesema:

“Muhammad ni mja Wake aliyeteuliwa.”

Yeye ni mja wa Allaah (´Azza wa Jall). Hana chochote katika haki ya uungu wala haki ya uola. Hakika si venginevyo yeye ni mja na Mtume wa Allaah anayetekeleza amri Zake, kujiepusha na makatazo Yake na mwenye kufikisha ujumbe kutoka kwa Allaah. Hapa wanaraddiwa wale wanaochupa mipaka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wako ambao wanachupa mipaka juu ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumfanya kuwa na baadhi ya sifa za uungu au uola na hivyo wakamuomba pamoja na Allaah. Huku ni kuchupa mipaka. Ni kama ambavyo manaswara walichupa mipaka kwa ´Iysaa bin Maryam  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Manaswara wamedai kuwa ´Iysaa ni mwana wa Allaah au yeye mwenyewe ndiye Allaah au watatu wa watatu. Hakika si venginevyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa ni mja. Kila kilichoko ardhini na mbinguni ni watumwa wa Allaah (´Azza wa Jall):

إِن كُلُّ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ إِلَّا آتِي الرَّحْمَـٰنِ عَبْدًا

“Hakuna yeyote yule aliyeko katika mbingu na ardhi isipokuwa atamjia ar-Rahmaan, hali ya kuwa ni mja.”[1]

Malaika pia ni waja:

بَلْ عِبَادٌ مُّكْرَمُونَ لَا يَسْبِقُونَهُ بِالْقَوْلِ وَهُم بِأَمْرِهِ يَعْمَلُونَ

“Bali ni waja waliokirimiwa. Hawamtangulii kwa kauli nao kwa amri Yake wanafanya.”[2]

Mitume na Manabii ni watumwa wa Allaah. Amesema (Subhaanah) kuhusu Nuuh (´alayhis-Salaam):

إِنَّهُ كَانَ عَبْدًا شَكُورًا 

“Hakika yeye alikuwa mja mwingi wa shukurani.”[3]

كَذَّبَتْ قَبْلَهُمْ قَوْمُ نُوحٍ فَكَذَّبُوا عَبْدَنَا وَقَالُوا مَجْنُونٌ وَازْدُجِرَ 

“Walikadhibisha kabla yao watu wa Nuuh, wakamkadhibisha mja Wetu wakasema: “Mwendawazimu” na akakaripiwa.”[4]

Amesema kuhusu Daawuud (´alayhis-Salaam):

اصْبِرْ عَلَىٰ مَا يَقُولُونَ وَاذْكُرْ عَبْدَنَا دَاوُودَ ذَا الْأَيْدِ ۖ إِنَّهُ أَوَّابٌ

“Subiri kwa yale wanayoyasema na mkumbuke mja Wetu Daawuud mwenye nguvu. Hakika yeye ni mwingi wa kutubia.”[5]

Amesema kuhusu Sulaymaan (´alayhis-Salaam):

وَوَهَبْنَا لِدَاوُودَ سُلَيْمَانَ ۚ نِعْمَ الْعَبْدُ ۖ إِنَّهُ أَوَّابٌ

“Daawuud Tukamtunuku Sulaymaan – uzuri ulioje wa mja! Hakika yeye ni mwingi wa kutubia.”[6]

Amesema kuhusu Ayyuub (´alayhis-Salaam):

وَاذْكُرْ عَبْدَنَا أَيُّوبَ إِذْ نَادَىٰ رَبَّهُ أَنِّي مَسَّنِيَ الشَّيْطَانُ بِنُصْبٍ وَعَذَابٍ

“Mkumbuke mja Wetu Ayyuub alipomuita Mola wake: “Hakika mimi amenigusa shaytwaan kwa tabu na adhabu.”[7]

Amesema kuhuu ´Iysaa (´alayhis-Salaam):

إِنْ هُوَ إِلَّا عَبْدٌ أَنْعَمْنَا عَلَيْهِ وَجَعَلْنَاهُ مَثَلًا لِّبَنِي إِسْرَائِيلَ

“Yeye si jengine isipokuwa ni mja Tuliyemneemesha na tukamfanya ni mfano kwa wana wa Israaiyl.”[8]

Ikiwa Mitume, Manabii na Malaika (ambao ndio viumbe watukufu zaidi wa Allaah) ni waja na watumwa wa Allaah, basi mawalii wengine wote wana haki zaidi.

[1] 19:93

[2] 21:26-27

[3] 17:3

[4] 54:9

[5] 38:17

[6] 38:30

[7] 38:41

[8] 43:59

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 57-58
  • Imechapishwa: 06/12/2022