Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah, Salaf, Kundi lililookoka na Kundi lililonusuriwa wanasimama upande wa watawala wa Kiislamu. Wanaridhia utawala wao kwa mujibu wa mipaka ya Shari´ah, wanawasikiliza na kuwatii hata kama itapigwa migongo yao na kuchukuliwa mali yao. Aidha wanawaombea du´aa ya kutengemaa. al-Fudhwayl bin ´Iyaadhw amesema:

“Ningelijua kuwa nina du´aa yenye kuitikiwa, basi ningelimuombea nayo mtawala.”[1]

Angelimuombea nayo mtawala na sio kujiombea mwenyewe. Mfano wa hayo yamesemwa na imamu wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah Ahmad bin Hanbal, mtunzi wa kitabu hichi chenye thamani. Kwa sababu mtu mwenye madaraka ana jukumu muhimu sana katika maisha ya mwanadamu.

Kwa maana hiyo ambaye anataka kumnasihi mtawala basi afanye hivo kwa njia sahihi. Akiweza kumtumia barua, afanye hivo. Akiweza kufanya hivo kwa mawasiliano, afanye hivo. Muhimu ni kuwa amnasihi kwa njia yoyote ya hekima na ya siri. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule anayetaka kumnasihi mtawala basi asifanye hivo hadharani. Badala yake amshike mkono wake na amnasihi chemba. Akiitikia, ni sawa, vinginevyo umetekeleza jukumu lako.”[2]

Ushauri kwa watawala unatofautiana na ushauri kwa watu wengine. Watawala wana nafasi za kipekee. Nasaha za siri na maalum zinapelekea katika manufaa ambayo hayapatikani kwa kuwanasihi hadharani. Ni makosa kiasi gani yanayofanywa na wale wanaosimama juu ya mimbari na kutaja makosa ya mtawala na makosa ya nchi hata kama ni kweli! Ni kosa kubwa sana. Mosi hakuondosha tatizo, pili hakubadilisha maasi kwa utiifu. Hakika hapana vyenginevyo alichofanya ni kuamsha fitina na kuwachochea wapumbavu dhidi ya mtawala. Matokeo yake kunazuka machafuko na fitina inaenea katika jamii. Kwa hiyo ni lazima kuwatii watawala wa Kiislamu, kuwasaidia katika utiifu na kuwavumilia. Kama alivosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Sikiliza na utii hata kama utapigwa mgongo wako na ikachukuliwa mali yako. Sikiliza na utii!”[3]

[1] Abu Nu´aym (8/91) na al-Khallaal (9).

[2] Ahmad (3/404), Ibn Abiy ´Aaswim (1096) na al-Haakim katika ”al-Mustadrak” (3/290). al-Haythamiy ameitaja katika ”Majma´-uz-Zawaa-id” (5/229) kwa tamko lisemalo ”Yule anayetaka kumnasihi… ”. Tamko hilo limepokelewa na al-Haakim na ni nzuri.

[3] Muslim (1847).

  • Muhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 113-114
  • Imechapishwa: 14/05/2026