‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anhaa) amesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alimteua bwana mmoja kuwa kiongozi wa msafara wa kijeshi. Yule mtu akawa anawaswalisha wenzake na akimalizia kwa:

قُلْ هُوَ اللَّـهُ أَحَدٌ

“Sema: ”Allaah ni Mmoja pekee.”[1]

Waliporudi wakamweleza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ambaye alisema: “Muulizeni ni kwa nini anafanya hivyo.” Wakamuuliza ambapo akajibu: “Kwa sababu ni sifa ya Mwingi wa rehema (´Azza wa Jall). Hivyo ndio maana napenda kuisoma.” Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Mwelezeni ya kwamba Allaah anampenda.”[2]

Hadiyth hii inafahamisha ukubwa wa kuziamini sifa za Mola, kuzipenda na kuwa na shauku ya kujifunza nazo na kwamba jambo hilo ni miongoni mwa sababu kubwa za kumwingiza mtu Peponi na kupata radhi za Mola (Subhaanah). ´Abdur-Razzaaq amesimulia kutoka kwa Ma´mar, kutoka kwa Ibn Twaawuus, kutoka kwa baba yake, ambaye amesimulia:

“Ibn ´Abbaas alimuona bwana mmoja akitetemeka hali ya kukataa wakati  aliposikia Hadiyth kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kuhusu sifa za Allaah, ambapo akasema: “Kipi kinachowatia khofu watu hawa? Wanapa ahueni wanaposikia zile Aayah zilizo wazi na wanaangamia wanaposikia zile Aayah zisizokuwa wazi.”

Sifa zote za Allaah ndani ya Qur-aan na Sunnah ziko wazi. Isipokuwa tu bwana huyu aliyetajwa kutokana na uchache wa elimu yake ndio akachanganya mambo na kuanza kukataa. Ndipo Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) akamkaripia na kumweleza kwamba ukataaji wake huu ni sababu ya kuangamia kwake. Tunacholenga kwa yote yaliyotangulia ni kwamba ni wajibu kuyaamini majina na sifa zote za Allaah zilizotajwa ndani ya Qur-aan na Sunnah. Imani hiyo imejumuishwa katika kumwamini Allaah na ni nguzo moja wapo ya kuwamini Allaah. Kwa sababu imani ya kumwamini Allaah inasimama juu ya nguzo tatu: kuamini kwamba Allaah yuko peke yake katika uola Wake, kuamini kuwa Allaah yuko peke yake katika kuabudiwa Kwake na kuamini kuwa Allaah yuko peke yake katika majina na sifa Zake.

[1] 112:1

[2] al-Bukhaariy (7375) na Muslim (813).

  • Muhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Allaamah ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad al-Badr
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Athar al-Mash-huur ´an-il-Imaam Maalik fiy Swifat-il-Istiwaa’, uk. 64-65
  • Imechapishwa: 04/12/2025