4 – Kichenguzi cha swawm aina ya nne ni kutoa damu kwa mwenye kufunga kwa kupiga chuku, kwa kupasua mshipa au kwa kuvuta damu kwa ajili ya kuchangia au kumuokoa mgonjwa na mfano wa hayo. Msingi wa hilo ni maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu kuumikwa:

”Amefungua mwenye kupiga chuku na mwenye kupigwa chuku.”[1]

Ameipokea Ahmad na at-Tirmidhiy.

Zimepokelewa Hadiyth nyingi kwa maana hii. Ibn Khuzaymah amesema:

”Hadiyth zimethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya hilo.”

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

”Maoni yanayosema kwamba kuumikwa kunafunguza ni maoni ya wengi wa wanazuoni wa Hadiyth akiwemo Ahmad, Ishaaq, Ibn Khuzaymah na Ibn-ul-Mundhir. Wanazuoni wa Hadiyth wanaofanyia kazi ndiyo watu waliobobea zaidi katika kumfuata Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Isitoshe maoni haya ndio yanayolingana na misingi ya Kishari´ah na kipimo. Ama wale ambao hawaonelei hivo wamejengea hoja kwa yale yaliyomo katika ”as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy; ya kwamba yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipiga chuku hali ya kuwa amefunga na akiwa katika Ihraam[2]. ´Abdullaah bin ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza:

”Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipiga chuku hali ya kuwa katika Ihraam na alipiga chuku hali ya kuwa ni mwenye kufunga.”

Ahmad na wengineo wameipinga ziada inayosema kuwa alikuwa amefunga na wakasema kwamba lililothibiti ni kuwa alipiga chuku akiwa ndani ya Ihraam. Ahmad amesema:

”… hali ya kuwa amefunga si sahihi.”

Mpaka pale Shaykh aliposema:

”Hili alilolitaja Ahmad ndilo walilokubaliana kwalo al-Bukhaariy na Muslim. Ndiyo maana Muslim alilipuuza na hakuthibitisha isipokuwa kupiga chuku kwa Muhrim.”

Ama kutoka damu bila kusudio la mfungaji ikiwa ni pamoja na kutokwa damu puani, damu ya jeraha, kung’olewa jino na mfano wa hayo, basi hilo halina athari juu ya swawm yake. Kwa sababu ana udhuru katika hali hizo. Lakini inampasa awe na tahadhari asimeze damu inayotoka kwenye jino au mfano wake.

[1] Abu Daawuud (2367), an-Nasaa´iy (3134), Ibn Maajah (1679-1681), Ibn Hibbaan (3532) na al-Haakim (01/427) ambaye amesema:

”Swahiyh kwa masharti ya al-Bukhaariy na Muslim.”

Vilevile na Ahmad (05/276).

[2] al-Bukhaariy (1938-139).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ithaaf Ahl-il-Iymaan bi Duruus Shahri Ramadhwaan, uk. 42
  • Imechapishwa: 13/03/2026