Haafidhw Ibn Hajar al-´Asqalaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:
23 – Jaabir bin ´Abdillaah (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:
“Mwaka ulipofunguliwa mji wa Makkah Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitoka kuelekea Makkah katika Ramadhaan. Watu walikuwa wamefunga. Mpaka alipofika Kuraa´-ul-Ghamiym akaomba chombo cha maji. Akakinyanyua ili watu wapate kumuona kisha akakinywa. Baada ya hapo akaambiwa kuwa kuna watu waliofunga ambapo akasema: “Hao ni waasi. Hao ni waasi.”
24 – Katika upokezi mwingine imekuja:
“Akaambiwa: “Baadhi ya watu swawm imekuwa ngumu kwao na wanasubiri waone utachofanya.” Ndipo akaomba chombo cha maji baada ya ´Aswr.”[1]
Ameipokea Muslim.
25 – Hamzah bin ´Amr al-Aslamiy amesema:
“Ee Mtume wa Allaah! Nahisi nguvu za kufunga safarini. Nina dhambi?” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ni ruhusa kutoka kwa Allaah. Yule mwenye kuitendea kazi amefanya vizuri na mwenye kupenda kufunga hakuna dhambi juu yake.”[2]
Ameipokea Muslim. Msingi wake ni kwa al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa ´Aaishah aliyesimulia kuwa Hamzah bin ´Amr alimuuliza.
MAELEZO
Katika Hadiyth hizi kuna dalili kwamba msafiri anaweza kufunga au kufungua, jambo ambalo ndio maoni ya kikosi kikubwa cha wanazuoni. Wamejengea hoja kwa Hadiyth ya Anas (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesema:
“Tulikuwa safarini pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi mwenye kufunga hakumlaumu mwenye kula, wala mwenye kula hakumlaumu mwenye kufunga.”[3]
Daawuud adh-Dhwaahiriy na Ibn Hazm wanaona kuwa swawm ya msafiri haisihi, bali alichoamrishwa ni kufungua[4], kwa sababu Allaah (Ta´ala) amesema:
فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ
“Basi atakayekuwa mgonjwa miongoni mwenu, au yuko safarini [akafunga baadhi ya siku], basi [akamilishe] idadi [ya siku anazotakiwa kufunga] katika siku nyinginezo.[5]
Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):
“Hao ni waasi. Hao ni waasi.”
Pia Hadiyth ya Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesema:
“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa safarini ambapo akaona msongamano na mtu ambaye ametengenezewa kivuli juu yake, akasema: ”Ni nini?” Wakasema: ”Ni mwenye kufunga.” Akasema: ”Si katika wema kufunga katika safari.”[6]
Sahihi ni maoni ya kwanza kutokana na nguvu ya dalili zake. Kuhusu Aayah haina dalili ya kwamba swawm ya msafiri haisihi ikiwa atafunga, bali inaonesha kwamba msafiri akila basi anatakiwa kufunga idadi ya siku katika siku nyingine. Sunnah inafafanua Qur-aan. Lau swawm katika safari ingelikuwa haisihi, basi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) asingelifanya wala yeyote miongoni mwa Maswahabah wake ambao ndio wenye elimu zaidi kuliko sisi kuhusu makusudio ya Allaah katika Kitabu Chake.
Isitoshe imepokelewa kutoka kwa baadhi ya Salaf katika Maswahabah na wanafunzi wao kwamba swawm safarini ni wajibu, kwa mujibu wa dhahiri ya maneno Yake Allaah (Ta´ala):
وَالْفُرْقَانِ ۚ فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ
“… na pambanuo [la haki na ubatilifu]. Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi [mpya] na afunge swawm.”[7]
Kuhusiana na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):
”Hao ni waasi.”
Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema juu ya wale walioenda kinyume ambao hawakutekeleza amri yake ya kufungua wakati swawm iliwalemea. Hapana shaka kwamba kufungua katika hali hii ni lazima. Aidha kutotii ni maasi. Kuhusu Hadiyth inayosema:
”Si katika wema kufunga katika safari.”[8]
alisema hivo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa yule swawm imemlemea kwa dalili ya mtiririko wake, kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifunga katika safari, ambaye hawezi kufanya lisilokuwa wema. Haki ni kwamba kusema kuwa kula safarini ni wajibu ni kupuuza Hadiyth zinazojulisha kufaa kufunga, nazo ni nyingi.
[1] Muslim (1114).
[2] al-Bukhaariy (1943) na Muslim (1121).
[3] al-Bukhaariy (1947) na Muslim (1118).
[4] al-Muhallaa (06/243).
[5] 02:184
[6] al-Bukhaariy (1946) na Muslim (1115).
[7] Tazama “Muswannaf” ya ´Abd-ur-Razzaaq” (04/269).
[8] al-Bukhaariy (1946) na Muslim (1115).
- Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
- Tarjama: Firqatunnajia.com
- Marejeo: Minhat-ul-´Allaam fiy Sharh Buluugh-il-Maraam (05/56-59)
- Imechapishwa: 26/02/2025
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window)
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window)
- Click to print (Opens in new window)
- Click to email a link to a friend (Opens in new window)
- Click to share on Facebook (Opens in new window)
- Click to share on Twitter (Opens in new window)
- Click to share on Pocket (Opens in new window)