41. Tafiti kuhusu kupangusa juu ya soksi za ngozi pea mbili

Tafiti ya pili inahusu pale ambapo anavaa soksi za juu ya soksi zengine. Jambo hili halitoki nje ya hali mbili:

Ya kwanza: Zile soksi za juu zimevaliwa baada ya kuchenguka kwa wudhuu´. Hapa hukumu itaambatana na zile za chini na wala asipanguse zile za juu.

Ya pili: Zile soski za juu zimevaliwa kabla ya kuchenguka kwa wudhuu´. Katika hali hii anayo khiyari. Akifuta zile soksi za chini basi hukumu itafungamana nazo na wala hakumdhuru kitu akivua zile za juu. Na kama atapangusa zile za juu basi hukumu itafungamana nazo. Kama atazivua basi atalazimika vilevile kuvua zile soksi za chini. Pale ambapo atapangusa moja wapo basi hukumu haitohama kwenda katika zile zengine. Haitosihi kuzipangusa wala zile za chini ikiwa ziko na matundu. Imekuja katika kitabu “al-Furuu´”:

“Asipanguse soksi za ngozi ambazo zimewekwa juu ya soksi za ngozi zengine zilizopanguswa… hata hivyo yale maoni yanayojuzisha yana mtazamo fulani, kama anavoonelea Maalik… “[1]

Katika kitabu hichohicho imekuja:

“Kama atavua zile soksi za ngozi za juu zilizopanguswa, Ahmad anaona kuwa atalazimika vilevile kuvua zile zilizoko chini. Hivyo mtu huyo atatawadha au ataosha miguu yake, jambo ambalo kuna tofauti juu yake. Ana maoni mengine yanayosema kuwa halazimiki kufanya hivo. Katika hali hiyo mtu huyo atatawadha au atafuta katika zile soksi zilizoko chini, jambo ambalo kuna tofauti juu yake.”[2]

Kutokana na maoni yanayosema kwamba uvuaji hauchengui twahara hakuna kitu kinachomlazimu mtu huyo.

Imekuja katika kitabu “al-Majmuu´” cha an-Nawawiy:

“Ikiwa tutajuzisha kupangusa juu ya gaita – ni kiatu ambacho huvaliwa juu ya soksi za ngozi na khaswa katika nchi za baridi – Abul-´Abbaas bin Surayj ametaja maana tatu juu ya hilo. Ya kwanza na ambayo ni sahihi zaidi ni kwamba zinachukua nafasi ya soksi za ngozi na soksi za ngozi zinachukua nafasi ya miguu. Ya pili ni kwamba zile za chini ni kama bendeji na zile za juu ni kama soksi za ngozi. Ya tatu ni kwamba ni kama soksi za ngozi moja; ile ya juu ni kama sehemu ya juu na ile ya chini ni kama seemu ya chini.”

Kutoka kwenye maana hizi wenzetu wametoa matawi mambo mengi. Moja wapo ni kwamba avue zile za juu baada ya kupangusa. Tukishikamana na ile maana ya kwanza, basi hatokuwa na haja ya kuvua zile za chini. Katika hali hiyo anaweza kuzipangusa. Lakini, je, inatosha kuzipangusa au ni lazima arudi kutawadha tena? Kuna maoni mawili juu ya mtu ambaye anavua soksi za ngozi. Na ikiwa tutashikamana na ile maana ya tatu basi hakuna kitu kinachomlazimu mtu huyo. Na ikiwa tutashikamana na ile maana ya tatu, basi italazimika avue zile za chini na aoshe miguu. Kuna maoni mawili kama anapaswa kutawadha upya. Kutokana na maoni mbalimbali juu ya mada hii kumezalikana maoni tatu:

1 – Hakuna kitu kinacholazimika.

2 – Yaliyo sahihi zaidi ni kufuta zile za chini peke yake.

3 –  Ni lazima kuzipangusa na kutawadha upya.

4 – Ni lazima kuvua soksi za ngozi na kuosha miguu.

5 – Ni lazima kuzivua na kutawadha upya.”[3]

Imekuja:

“Kama mtu atavua soksi za ngozi akiwa na twahara, wudhuu´ wake ukachenguka, akazipangusa kisha akavaa gaita, kuna maoni mawili yanayotambulika kama inafaa kupangusa juu yake.”[4]

Kisha akasema kuwa maoni yanayojuzisha ndio yanayoonekana kuwa ya sawa kwa sababu amevaa gaita akiwa na wudhuu´:

“Fikira yao kwamba ni twahara pungufu ni jambo la kimakosa. ar-Raafi´iy ameeleza kwamba Shaykh Abu ´Aliy amesema: “Ikiwa tutasema kuwa inafaa kupangusa katika hali hii, basi muda wa kupangusa unaanza kuhesabiwa kuanzia kuanzia pale wudhuu´ unapochenguka baada ya kuzivaa soksi za ngozi na si baada ya kuvaa gaita.”[5]

Maoni yanayosema kuwa muda wa kupangusa unaanza kuanzi pale twahara inapochenguka yatatajwa.

[1] al-Furuu´ (1/160).

[2] al-Furuu´ (1/172).

[3] al-Majmuu´ (1/490).

[4] al-Majmuu´ (1/490).

[5] al-Majmuu´ (1/490).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Buhuuth wa Fataawaa fiyl-Mas´h ´alaal-Khuffayn, katika Majmuu´-ul-Fataawaa (11/184-185)
  • Imechapishwa: 11/05/2021