Kwa mnasaba huu tunalazimika kubainisha aina za Tawassul zinazofaa na Tawassul zisizofaa. Kuna aina mbili za Tawassul imegawanyika sehemu mbili; Tawassul zinazofaa na Tawassul zilizokatazwa. Kuna aina mbalimbali ya Tawassul zinazofaa ikiwa ni pamoja na:

1- Kutawassul kwa Allaah kwa majina na sifa Zake (Subhaanahu wa Ta´ala). Amesema (Ta´ala):

وَلِلَّـهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ فَادْعُوهُ بِهَا ۖ وَذَرُوا الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي أَسْمَائِهِ ۚ سَيُجْزَوْنَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ

”Allaah ana majina mazuri kabisa. Hivyo basi, muombeni kwayo. Waacheni wale wanaopotoa/haribu katika majina Yake. Watalipwa yale waliyokuwa wakiyatenda.” (al-A´raaf 07:180)

Muombeni kwayo – Bi maana mtawassul kwayo kwa Allaah. Kwa mfano kusema: “Ee ar-Rahmaan! Nirehemu!”, “Ee al-Ghafuur! Nisamehe!”, “Ee al-Kariym! Nikirimu na unipe!”, “Ee al-Ghaniy! Nitajirishe!” na mengineyo. Unamuomba Allaah (´Azza wa Jall), unatawassul Kwake wa majina Yake. Kama jinsi alivyotawassul Ayyuub (´alayhis-Salaam) pale aliposema:

وَأَيُّوبَ إِذْ نَادَىٰ رَبَّهُ أَنِّي مَسَّنِيَ الضُّرُّ وَأَنتَ أَرْحَمُ الرَّاحِمِينَ

”Ayyuub alipomwita Mola wake [huku akiomba]: “Hakika mimi imenigusa dhara Nawe ni mbora wa wanaorehemu.” (al-Anbiyaa´ 21:83)

Ametawassul kwa Allaah kwa kuwa Allaah ni mbora wa wanaorehemu. Allaah akampokelea du´aa yake.

Yuunus (´alayhis-Salaam) katawassul, naye alikuwa ndani ya tumbo la chewa na ndani ya viza; giza la bahari, giza la usiku na giza la tumbo la chewa:

فَنَادَىٰ فِي الظُّلُمَاتِ أَن لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنتَ سُبْحَانَكَ إِنِّي كُنتُ مِنَ الظَّالِمِينَ فَاسْتَجَبْنَا لَهُ

“Akaita katika visa kwamba: “Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Wewe, kutakasika kutokamana na mapungufu ni Kwako! Hakika mimi nimekuwa miongoni mwa madhalimu.” Basi Tukamuitikia.” (al-Anbiyaa´ 21:87-88)

Ametawassul kwa Allaah kwa Tawhiyd. Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Wewe. Ametawassul kwa Allaah kwa kutambua dhambi yake:

إِنِّي كُنتُ مِنَ الظَّالِمِينَ

“Hakika mimi nimekuwa miongoni mwa madhalimu.”

Allaah akamuitikia.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 68-69
  • Imechapishwa: 11/08/2018