40. Usafishaji wa mdomo kwa ajili ya kusoma Qur-aan

Yule anayetaka kusoma Qur-aan anatakiwa kusafisha mdomo wake kwa Siwaak au vinginevyo. Lililo chaguo katika Siwaak ni iwe kwa kijiti cha mti wa Salvadoraceae (أراك). Hata hivyo inajuzu kwa miti mingine yote na kwa kila kinachosafisha kama kitambaa kigumu, mimea mingine na vinginevyo.

Kuhusu utumiaji wa kidole gumba kuna maoni matatu kwa wafuasi wa ash-Shaafi´iy (Rahimahumu Allaah):

1 – Haisihi.

2 – Inasihi.

3 – Inasihi ikiwa hakupata kingine na haisihi ikiwa amepata.

Apige Siwaak kwa upana hali ya kuanza kwa upande wa kulia wa mdomo wake na anuie kwa hilo kufanyia kazi Sunnah. Baadhi ya wanazuoni wamesema: ”Aseme wakati wa kupiga Siwaak:

اللهم بارك لي فيه يا أرحم الراحمين

“Ee Allaah! Nibarikie kwayo! Ee Mwenye rehema zaidi ya wenye kurehemu!”

al-Maawardiy, ambaye ni miongoni mwa wafuasi wa ash-Shaafi´iy, amesema ya kwamba inapendekezwa apige Siwaak upande wa nje wa meno yake na ndani yake, apitishe Siwaak juu ya ncha za meno yake, magego ya meno ya nyuma na juu ya paa la koo lake kwa upole.”

Aidha wamesema kwamba inapasa atumie Siwaak wa kati, usiwe mgumu sana wala laini sana. Ikiwa utakuwa mgumu sana, ulainishwe kwa maji. Hakuna ubaya kutumia Siwaak ya mwingine kwa idhini yake.

Ama ikiwa mdomo wake una najisi kama damu au kinginecho, basi inachukiza kwake kusoma Qur-aan kabla ya kuuosha. Je, ni haramu? ar-Ruwayaaniy  amesema, ambaye ni miongoni mwa wafuasi wa ash-Shaafi´iy, amesimulia kutoka kwa baba yake aliyesema kuwa madhehebu yana maoni mawili katika suala hili na sahihi zaidi ni kwamba si haramu.

  • Muhusika: Imaam Yahyaa bin Sharaf an-Nawawiy (afk. 677)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tibyaan fiy Aadaabi Hamalat-il-Qur-aan, uk. 49
  • Imechapishwa: 26/08/2026