Ahl-ul-Hadiyth wanathibitisha ukhaliyfah wa Abu Bakr (Radhiya Allaahu ´anh) baada ya kufa kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Alichaguliwa na Maswahabah na wakaafikiana juu yake. Wote walisema:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuridhia juu ya dini yetu, na sisi tunakuridhia juu ya dunia yetu.”

Bi maana yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alichukau nafasi yake ya kuwaswalisha watu swalah za faradhi kipindi cha maradhi yake. Jambo hilo ndio dini. Kwa ajili hiyo tumekuridhia kama khaliyfah wake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika dunia yetu. Walisema tena:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekutanguliza mbele, ni nani atayekurdisha nyuma?”

Walichokusudia ni kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimtanguliza mbele kuswalisha wakati alipokuwa mgonjwa. Tukaswali nyuma yako kwa amri yake; ni nani ambaye atakurudisha nyuma baada ya yeye kukutanguliza mbele?

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati wa uhai wake alikuwa akimzungumza Abu Bakr mbele ya Maswahabah kwa njia inayowabainikia ya kwamba yeye ndiye mtu mwenye haki zaidi ya ukhaliyfah baada yake. Kwa ajili hiyo wakakubaliana na kukusanyika juu yake. Naapa kwa Allaah! Wakanufaika na wakanyanyuka sana kutokana na nafasi yake. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Naapa kwa Yule ambaye hapana mungu wa haki mwingine asiyekuwa Yeye! Kama Abu Bakr asingelifanywa khaliyfah, basi asingeliabudiwa Allaah.”

Wakati walipopingana na maneno yake, akayasimamishia hoja na dalili maneno yake ambapo wakamsadikisha na kumkubalia maneno yake.

Baada ya hapo kunafuatia ukhaliyfah wa ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh). Abu Bakr (Radhiya Allaahu ´anh) ndiye alimteua kuchukua nafasi yake. Aidha Maswahabah waliafikiana juu yake baada yake. Kupitia yeye Allaah (Subhaanah) alitimiza ahadi Yake ya utawala wa Uislamu na ukuu wake.

Halafu ukafuatia ukhaliyfah wa ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh) kwa maafikiano ya watu wa Mashauriano na Maswahabah wote kwa jumla. Walimridhia kiasi cha kwamba wakampa kazi hiyo yeye.

Kisha ukhaliyfah wa ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh). Ulithibiti kwa kiapo cha Maswahabah kwake. Wote walijua na wakaona kuwa yeye (Radhiya Allaahu ´anh) ndiye kiumbe ambaye ana haki na kustahiki zaidi ya ukhaliyfah katika wakati huo. Hawakujuzisha kuasiwa na kwenda kinyume naye.

Hawa ndio makhaliyfah wanne waongofu ambao Allaah ameinusuru, kuwatisha wakanamungu na akautia nguvu Uislamu kupitia wao. Kipindi chao haki ikashinda. Nuru, mwangaza wao uliangaza giza. Kwa ukhaliyfah wao ikahakiki ahadi Yake iliyotangulia:

وَعَدَ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَيَسْتَخْلِفَنَّهُمْ فِي الْأَرْضِ كَمَا اسْتَخْلَفَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ وَلَيُمَكِّنَنَّ لَهُمْ دِينَهُمُ الَّذِي ارْتَضَىٰ لَهُمْ وَلَيُبَدِّلَنَّهُم مِّن بَعْدِ خَوْفِهِمْ أَمْنًا ۚ يَعْبُدُونَنِي لَا يُشْرِكُونَ بِي شَيْئًا

“Allaah amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na wakatenda mema kwamba atawafanya makhalifa katika ardhi – kama alivyowafanya makhalifa wale waliokuwa kabla yao – na atawamakinishia dini yao aliyowaridhia na atawabadilishia amani badala ya khofu yao – [kwa sharti] wananiabudu Mimi na hawanishirikishi na chochote.”[1]

مُّحَمَّدٌ رَّسُولُ اللَّـهِ ۚ وَالَّذِينَ مَعَهُ أَشِدَّاءُ عَلَى الْكُفَّارِ رُحَمَاءُ بَيْنَهُمْ

”Muhammad ni Mtume wa Allaah na wale walio pamoja naye ni wakali kwa makafiri wanahurumiana baina yao.”[2]

Kwa hivyo yule atakayewapenda, akasimama upande wao, akawaombea, akachunga haki zao na akatambua fadhilah zao,  basi huyo ni katika waliofuzu. Yule ambaye atawabughudhi, akawachukia na kuwatuhumu yale wanayowatuhumu Raafidhwah na Khawaarij, basi ameangamia. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Msiwatukane Maswahabah wangu[3]. Yule mwenye kuwatukana Maswahabah wangu Allaah amemlaani[4].”

Amesema tena (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Yule mwenye kuwapenda, amewapenda kwa sababu ya kunipenda. Yule mwenye kuwabughudhi, amewabughudhi kwa kunibughudhi. Yule mwenye kuwaudhi, ameniudhi. Yule mwenye kuwatukana Allaah amemlaani.”[5]

[1] 24:55

[2] 48:29

[3] al-Bukhaariy (3673) na Muslim (2540).

[4] al-Haakim (2/483).

[5] at-Tirmidhiy (3862) na Ahmad (16361). Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Dhwa´iyf-ul-Jaamiy´” (1160).

  • Mhusika: Imaam Abu ´Uthmaan Ismaa´iyl bin ´Abdir-Rahmaan as-Swaabuuniy (afk. 449)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-us-Salaf wa Aswhaab-il-Hadiyth, uk. 289-294
  • Imechapishwa: 25/12/2023