40. Mwenye hedhi na mwenye nifasi wakitwahirika mchana au usiku wa Ramadhaan

Hedhi ni damu ya kimaumbile inayomjia mwanamke katika masiku maalum. Ikimtokea hedhi ilihali amefunga – ijapokuwa ni muda mfupi kabla ya jua kuzama – basi swawm yake ya siku hiyo itaharibika na atalazimika kulipa. Isipokuwa ikiwa kama funga yake ni ya sunnah basi hapo kulipa kwake kutapendekezwa na si lazima.

Akisafika na hedhi katikati ya mchana wa Ramadhaan basi haitosihi swawm yake masaa mengine yaliyobaki siku hiyo kwa kupatikana kinachopingana na swawm yake katika haki yake sehemu ya mwanzo ya mchana. Je, ni lazima kwake kujizuia masaa mengine yaliyobaki siku hiyo? Wanachuoni wametofautiana, jambo ambalo tumekwishatangulia kulitaja kuhusu msafiri akifika katika mji wake hali ya kuwa hakufunga.

Akisafika usiku katika Ramadhaan – ijapo ni kipindi kifupi kabla ya kuchomoza kwa alfajiri – basi ni lazima kwake kufunga. Kwa sababu ni katika watu wanaoguswa na funga na hakuna kinachomkosesha kufanya hivo. Kwa hiyo itawajibika kwake kufunga na hapo swawm yake itasihi ingawa hatooga isipokuwa baada ya kupambazuka alfajiri. Ni kama mfano wa mwenye janaba akifunga na asioge isipokuwa baada ya kuingia alfajiri. Yeye pia swawm yake inasihi. Hilo ni kutokana na maneno ya ´Aishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliyesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiamka na janaba, inayotokana na jimaa na si kuota, kisha anafunga katika Ramadhaan.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Mwanamke mwenye damu ya uzazi ana hukumu moja kama mwenye hedhi katika yale yote yaliyotangulia.

Ni lazima kwao wote wawili kulipa idadi ya siku zilizowapita. Amesema (Ta´ala):

فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

“… hivyo basi akamilishe idadi katika siku nyinginezo.”[1]

´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliulizwa:

“Mbona mwenye hedhi analipa funga na wala halipi swalah?” Akajibu: “Hali hiyo ilikuwa ikitupata na tunaamrishwa kulipa swawm na wala hatuamrishwi kulipa swalah.”

Ameipokea Muslim.

[1] 02:184

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 56-58
  • Imechapishwa: 08/05/2020