40. Jibu zuri sana na imara la jumla dhidi ya mshirikina

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Hili ni jibu zuri sana na imara, lakini hakuna anayelifahamu isipokuwa yule ambaye amewafikishwa na Allaah. Hivyo, usilidharau. Kwa hakika Allaah (Ta´ala) anasema:

وَمَا يُلَقَّاهَا إِلَّا الَّذِينَ صَبَرُوا وَمَا يُلَقَّاهَا إِلَّا ذُو حَظٍّ عَظِيمٍ

“Na hawatopewa [sifa hii] isipokuwa wale waliovuta subira, na hapewi hayo isipokuwa mwenye fungu kubwa.” (41:35)

MAELEZO

Bi maana mtu kumwambia mpinzani kuwa maneno ya Allaah (Ta´ala) hayagongani kabisa, na kwamba maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hayapingani na maneno ya Allaah na kwamba jambo la wajibu ni kuzirudisha Aayah zenye kutatiza katika Aayah zilizo wazi. Hili ni jibu zuri sana na imara, kwa kuwa hakuna awezaye kuyapinga au kuyaraddi kwa kitu chenye kuyabatilisha. Hilo ni kwa sababu ni jibu lililojengwa juu ya dalili mbili; ya Kishari´ah na ya kiakili. Kwa ajili hiyo ni jibu ambalo hakuna mtu wa batili awezaye kulibatilisha.

Mtunzi (Rahimahu Allaah) amesema:

“… lakini hakuna anayelifahamu isipokuwa yule ambaye amewafikishwa na Allaah… “

Jibu hili linafahamika na yule ambaye Allaah amemuwafikisha. Amemuokoa na mtihani wa hoja tata na fitina ya matamanio. Kisha akatoa dalili kwa maneno Yake (Ta´ala):

وَمَا يُلَقَّاهَا إِلَّا الَّذِينَ صَبَرُوا

“Na hawatopewa [sifa hii] isipokuwa wale waliovuta subira.”

Bi maana yule ambaye amewafikishwa peke yake ndiye ambaye anaweza kuraddi kwa njia iliokuwa bora.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 59-60
  • Imechapishwa: 11/11/2023