Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ ۗ يُرِيدُ اللَّـهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ

“Na atakayekuwa mgonjwa au safarini basi [atimize] idadi katika siku nyinginezo. Allaah Anakutakieni mepesi na wala Hakutakieni magumu.” (02:185)

Kuna aina mbili ya wagonjwa:

Ya kwanza: Magonjwa sugu yenye kuendelea kama mfano wa kansa. Katika hali hii mgonjwa sio lazima kufunga kwa sababu maradhi yake ni sugu. Badala yake anatakiwa kwa kila siku moja kulisha masikini. Chaguo la kwanza anaweza kuwakusanya masikini wote kwa wakati mmoja na kuwapa chakula cha jioni au cha mchana. Hivyo ndivyo alivofanya Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) wakati alipokuwa mzee. Chaguo lingine ni yeye kutoa ngano nzuri gramu 510  kumpa masikini kwa kila siku moja ambayo haikufungwa. Ikiwa ataongezea juu ya hilo nyama au mafuta ni vizuri. Hukumu hiyo hiyo inamuhusu mzee asiyeweza kufunga.

Ya pili: Magonjwa yasiyokuwa sugu kama mfano wa homa. Hapa kuna hali tatu:

1- Swamw haimtii uzito wala haimdhuru mfungaji. Hapa ni wajibu kwake kufunga kwa sababu hana udhuru wowote.

2-  Swawm inamtia uzito mgonjwa pasina kumdhuru. Hapa imechukizwa kufunga kwa sababu  ameacha kuchukua rukhusa ya Allaah (Ta´ala) na kujiwekea uzito mwenyewe.

3- Swamw inamtia uzito na kumdhuru mgonjwa. Hapa itakuwa ni haramu kufunga kwa sababu ni kujiweka katika madhara. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَا تَقْتُلُوا أَنفُسَكُمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِكُمْ رَحِيمًا

“Wala msijiue. Hakika Allaah daima kwenu ni Rahiymaa, Mwenye kurehemu.” (04:29)

وَلَا تُلْقُوا بِأَيْدِيكُمْ إِلَى التَّهْلُكَةِ

“Wala msijitupe kwa mikono yenu katika maangamizi.” (02:195)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna madhara, wala kudhuriana.”[1]

Ameipokea Ibn Maajah na al-Haakim.

an-Nawawiy amesema:

“Imepokelewa kwa njia nyingi zenye kupeana nguvu.”

Mgonjwa hujua kama maradhi yanamdhuru kupitia hisia zake mwenyewe au madaktari waaminifu. Mgonjwa aliye na aina ya maradhi haya anatakiwa kulipa yale masiku aliyokula wakati atapopona. Akifa kabla ya kupona uwajibu wake umeanguka.

Kuna aina mbili ya wasafiri:

Ya kwanza:  Msafiri mwenye kusafiri ili akwepe swawm. Hapa itakuwa bado ni wajibu kwake kufunga. Ujanja haufanyi faradhi za Allaah zikaanguka.

Ya pili: Msafiri asiyekusudia hilo. Hapa kuna hali tatu:

1- Safiri ikawa inamtia uzito mkubwa. Hapa itakuwa ni haramu kwake kufunga. Pindi Mtume (Swalla Allahu ´alayhi wa sallam)  alipokuwa katika kuifungua Makkah alifunga ambapo akapata khabari ya kwamba kuna watu ambao wanatatizwa na swawm na kwamba wanasubiri tu waone nini atakachofanya. Hivyo baada ya ´Aswr, akaomba chombo cha maji na akanywa na huku watu wanamtazama. Kukasemwa kuambiwa kuwa kuna watu ambao bado wameendelea kufunga ambapo akasema:

“Hao ni watenda madhambi, hao ni watenda madhambi.”[2]

Imepokelewa na Muslim.

2- Safiri ikawa haimtii uzito sana mfungaji. Hapa imechukizwa kufunga kwa sababu ya kuacha kuchukua rukhusa ya Allaah (Ta´ala) na mtu kujitia uzito mwenyewe.

3- Safiri ikawa si yenye kumtia uzito mfungaji. Hapa ana khiyari ya kufanya lile aonalo kuwa ni lepesi kwake. Allaah (Ta´ala) amesema:

يُرِيدُ اللَّـهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ

“Allaah Anakutakieni mepesi na wala Hakutakieni magumu.” (02:185)

Kutaka hapa kunamaanishwa kupenda. Akiona kuwa yote mawili ni sawa kwake, basi kufunga ni bora kwake kwa sababu ndio ilikuwa kitendo cha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kuwa Abud-Dardaa´ (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Tulisafiri pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Ramadhaan wakati kulipokuwa na joto kali mpaka tukawa tumeweka mikono yetu kichwani kwa sababu ya ukali wa joto. Hakuna aliyekuwa amefunga kati yetu isipokuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ´Abdullaah bin Rawaahah.”[3]

Msafiri anakuwa katika safari tokea pale anapotoka nje ya mji wake mpaka pale ataporudi. Hata kama atakaa katika mji aliouendea kwa muda mrefu bado yumo safarini maadamu ananuia kurudi pale ambapo haja yake itakuwa imeisha. Kwa sababu haikuthibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutenga muda maalum. Asli ni kubaki kwa safari na hukumu zake mpaka kuthibiti dalili zenye kuonesha kinyume.

Haijalishi kitu safari ikiwa ni ya muda kama Hajj, ´Umrah, kuwatembelea ndugu, biashara au safari ni ya kuendelea kama safari ya teksi [tax] au safari za magari makubwa makubwa [lori]. Wakati wanapotoka katika miji yao ni wasafiri na hivyo inajuzu kwao kufanya yale yote wasafiri wengine wanapata kufanya katika kula, kufupisha swalah ambazo ni za Rakaa nne na kujumuisha Dhuhr na ´Aswr na Maghrib na ´Ishaa wakati wa haja. Ikiwa ni sahali kwao kutokufunga basi ni bora kwao kutokufunga. Badala yake watazilipa katika majira ya baridi. Kwa sababu madereva hawa wana miji yao wanapoeshi. Wanapokuwa katika miji yao ni wakazi na hivyo wazingatie zile sheria zenye kuwagusa wakazi. Na pindi wanaposafiri wao ni wasafiri na hivyo wazingatie zile sheria zenye kuwagusa wakazi.

[1] Ibn Maajah (2341), Ahmad (5/327) na al-Haakim (2345).

[2] Muslim (1114).

[3] Muslim (1122).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Utaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fusuwl fiys-Swiyaam wat-Taraawiyh waz-Zakaah, uk. 7-9
  • Imechapishwa: 03/06/2017