Moja katika majina ya Allaah (Ta´ala) ni mwingi wa Hekima, al-Hakiym. Mwingi wa Hekima ni yule mwenye kusifika na hekima. Hekima maana yake ni kuwa bingwa wa yote na kuyaweka mambo mahala pake stahiki. Kwa vile Allaah (Ta´ala) anaitwa hivyo hili linapelekea yote Anayoumba au kuyaweka katika Shari´ah yatokamane na hekima iliyopindukia. Kuna wenye kuyajua hayo, na wasioyajua.

Swawm ambayo Allaah ameiweka katika Shari´ah na kuwafaradhishia nayo waja Wake ina hekima kubwa na faida nyingi ikiwa ni pamoja na:

1- Swawm ni ´ibaadah. Mja anajikurubisha kwa Mola Wake kwa kuacha vile anavyovipenda katika vyakula, vinywaji na jimaa si kwa jengine isipokuwa tu ni kwa sababu aweze kupata radhi na Pepo ya Mola Wake. Hilo linafahamisha kuwa amezipa kipaumbele radhi za Allaah na nyumba ya Aakhirah juu ya matamanio yake.

2- Swawm ni sababu ya [kuapata] taqwa. Allaah (Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

“Enyi mlioamini! Mmeandikiwa [fardhi ya] swawm kama ilivyoandikwa kwa walio kabla yenu mpate kuwa na taqwa.” (02:183)

Mfungaji ameamrishwa kumcha Allaah (´Azza wa Jall). Taqwa maana yake ni kutekeleza maamriho Yake na kujiepusha na makatazo Yake. Hayo ndio malengo makubwa ya swawm. Malengo sio kumuadhibu mfungaji kwa kushinda na njaa, kiu na kufanya jimaa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah hana haja kwa mtu kuacha chakula na kinywaji chake ikiwa haachi uongo na kufanya matendo ya uongo huo na madhambi.”[1]

Imepokelewa na al-Bukhaariy.

Uongo inahusu maneno yote yaliyoharamishwa kama vile porojo, usengenyaji, matusi na mfano wa hayo. Kufanya matendo ya uongo huo maana yake ni matendo yote ambayo ni mashambulizi kwa watu kama vile khiyana, usaliti, kipigo, wizi na mfano wa hayo. Ndani yake kunaingia vilevile yale yote yaliyoharamishwa kusikiliza kama vile muziki na ala za muziki.

Madhambi ni upumbavu na kila kinachopingana na usalama wa maneno na vitendo.

Lau mfungaji atafanyia kazi Aayah hii na Hadiyth hii basi swawm itamlea nafsi yake, kusafisha tabi yake na kurekebisha mwenendo wake. Kwa hiyo swawm mwishoni wa Ramadhaan itakuja kumuathiri kwa hali ya juu inapokuja kwake mwenyewe, tabia yake na mwenendo wake.

3- Tajiri huona neema ya Allaah aliyopewa pale ambapo yuko na uwezo wa kula na kunywa akitakacho na kufanya jimaa kwa njia ya halali. Hivyo amshukuru Allaah kwa neema hii na kumfikiria ndugu yake fakiri asiyekuwa na uwezo huo. Kwa ajili hiyo ampe swadaqah na kumtendea wema.

4- Swawm inaipa nafsi mazoezi ya kushika adabu ili iweze kukabiliana na yale yenye kuipa mafanikio duniani na Aakhirah. Swawm inamkinga mtu na mwenendo wa kinyama ambao hauwezi kujizuia na shahawa na matamanio. Ni kitu kinachoinufaisha nafsi.

5- Swawm inapalekea vilevile kupatikana kwa faida za kiafya. Mwili unapewa chakula kidogo na utumbo unatumia fursa ya kupata nafuu kwa muda maalum. Kadhalika rutuba zenye madhara na mafuta yanasafishwa na mengineyo.

[1] al-Bukhaariy (1903).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Utaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fusuwl fiys-Swiyaam wat-Taraawiyh waz-Zakaah, uk. 5-6
  • Imechapishwa: 03/06/2017