39. Ni sawa kulengesha kuwa usiku wa Qadar ni tarehe 27?

Swali 39: Baadhi ya waislamu wamezowea na kusifu usiku wa tarehe ishirini na saba kwamba ndio usiku wa Qadar. Je, malengesho haya yana msingi wowote na ni ipi dalili?

Jibu: Ndio, malengesho haya yanayo msingi. Usiku wa tarehe ishirini na saba ndio kuna matarajio zaidi ya kuweko usiku wa Qadar. Hayo yametajwa katika “as-Swahiyh” ya Muslim kupitia kwa Ubayy bin Ka´b (Radhiya Allaahu ´ann). Lakini hata hivyo maoni yenye nguvu ya wanachuoni ambayo yamefika zaidi ya arobaini ni kwamba usiku wa Qadar unakuwa katika yale masiku kumi ya mwisho na khaswa katika zile siku saba za mwisho. Usiku wa Qadar unaweza kuwa tarehe ishirini na saba, ishirini na tano, ishirini na tatu, ishirini na tisa, ishirini na nane, ishirini na sita na pia unaweza kuwa usiku wa tarehe ishirini na nne. Kwa ajili hiyo basi mtu anatakiwa kujipinda katika kila usiku ili asikose fadhilah na ujira wake. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةٍ مُّبَارَكَةٍ ۚ إِنَّا كُنَّا مُنذِرِينَ

“Hakika Sisi tumeiteremsha katika usiku uliobarikiwa – hakika Sisi daima ni Wenye kuonya [watu].”[1]

إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةِ الْقَدْرِ وَمَا أَدْرَاكَ مَا لَيْلَةُ الْقَدْرِ  لَيْلَةُ الْقَدْرِ خَيْرٌ مِّنْ أَلْفِ شَهْرٍتَنَزَّلُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ فِيهَا بِإِذْنِ رَبِّهِم مِّن كُلِّ أَمْرٍ سَلَامٌ هِيَ حَتَّىٰ مَطْلَعِ الْفَجْرِ

“Hakika Sisi tumeiteremsha Qur-aan katika usiku wa Qadr. Na kipi kitakachokujulisha ni nini huo usiku wa Qadr? Usiku wa Qadr ni mbora kuliko miezi elfu: wanateremka humo Malaika na Roho kwa idhini ya Mola wao kwa kila jambo. Ni amani mpaka kuchomoza alfajiri!”[2]

[1] 44:03

[2] 97:01-05

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: 48 mas-alatu fiy Swiyaam, uk. 36-37
  • Imechapishwa: 28/04/2021