Wanazuoni wametumia kipimo ya kula na kunywa vifunguzi vingine. Hilo ni kutokamana na maneno yake katika riwaya ya pili:

“Mwenye kufungua katika Ramadhaan kwa kusahau basi hakuna juu yake kulipa wala kafara.”[1]

Kutajwa kwa kula na kunywa katika Hadiyth hii ni kwa sababu hiyo ndiyo hali inayotokea mara nyingi, na kutenga hukumu kwa jambo fulani kwa kutegemea hali ya kawaida haimaanishi kuwa hukumu hiyo haipo kwa mambo mengine yanayofanana nayo. Kwa hiyo hukumu hii kwa mwenye kufunga ni sehemu ya kanuni kuu inayojulishwa na maneno Yake (Ta´ala):

رَبَّنَا لَا تُؤَاخِذْنَا إِن نَّسِينَا أَوْ أَخْطَأْنَا

“Ee Mola wetu! Usituchukulie pale tutaposahau au tukikosea.”[2]

Imesihi ya kwamba Allaah (Ta´ala) amesema hali ya kujibu du´aa hii:

”Nimekwishafanya.”

Imekuja katika upokezi mwingine:

”Ndio.”[3]

Hii ni katika rehema, upole, wepesi Wake kwa waja, kuwaondoshea uzito na mashaka juu yao.

Katika hukumu hiyo pia inajumuishwa hali zifuatazo ikiwa mwenye kufunga ataoga, atasukutua mdomo au ataingiza maji puani, kisha maji yakaingia kooni mwake bila ya kukusudia, basi swawm yake haibatiliki. Vivyo hivyo ikiwa nzi, vumbi au unga utaingia kooni mwake bila kutaka kwake, basi swawm yake haibatiliki, kwa sababu hali hii inafanana na msahau katika maana ya kutokukusudia na kutokuwa na khiyari.

Mtu akimuona mwenye kufunga anakula au anakunywa katika mchana wa Ramadhaan kwa kusahau, ni lazima amkumbushe na kumjulisha mara moja. Kwa sababu kufanya hivo ni kwa minajili ya kuamrisha mema na kukataza mabaya. Kula na kunywa katika mchana wa Ramadhaan ni maovu, hata kama mwenye kufanya hivyo amesamehewa. Hivyo ikawajibika kumkumbusha – na Allaah ndiye mjuzi zaidi.

[1] al-Haakim (1/430).

[2] 02:286

[3] Muslim (199-200).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Minhat-ul-´Allaam fiy Sharh Buluugh-il-Maraam (05/51-52)
  • Imechapishwa: 24/02/2025