Sifa mbili hizi zinapatikana kwa wale wanazuoni wetu walioharibika wanaofanana na watu wa Kitabu:

1 – Wanayapotosha maneno. Hakika yule ambaye anasoma kwa lengo jengine lisilokuwa matendo moyo wake unakuwa msusuwavu na hivyo matokeo yake hajishughulishi na matendo. Badala yake anakuwa mwenye kukengeusha maneno na kupindisha matamko ya Qur-aan na Sunnah kutoka mahala pake stahiki kwa kutafuta msaada wa vichochoro vya mafumbo ya lugha na mifumo mingine iliombali. Aidha kuyaponda matamshi ya Sunnah kwa vile hawawezi kufanya hivo kwa matamshi ya Qur-aan. Wanawasema vibaya wale wenye kushikamana na Qur-aan na Sunnah kidhahiri na kuwavugumizia tuhuma za ujinga na wasiokuwa na maana yoyote. Sifa hii inapatikana kwa wanafalsafa, wanazuoni wa Rai (أهل الرأي) na wanafalsafa wa kisufi na mutakallimiyn.

2 – Wanasahau ile elimu yenye manufaa waliyokumbushwa na kwa ajili hiyo nyoyo zao haziwaidhiki. Badala yake wanawasema vibaya wale wenye kujifunza mambo yenye kuwafanya kulia na kuzilainisha nyoyo zao na kuwatuhumu ugumu. Watu wa rai wamewanukuu wanazuoni wao namna ambavyo matunda ya elimu yanajulisha utukufu wa elimu hizo. Wanachomaanisha ni kwamba yule mwenye kujishughulisha na kuifasiri Qur-aan kubwa analofikia ni kuwasilimulia watu elimu yake, ilihali yule mwenye kujishughulisha na yale waliyoonelea wao na elimu yao basi anayo haki ya kufutu, kumua, kuhukumu na kufunza. Watu hawa wanakumbushia wale waliotajwa katika:

يَعْلَمُونَ ظَاهِرًا مِّنَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَهُمْ عَنِ الْآخِرَةِ هُمْ غَافِلُونَ

“Wanajua ya juujuu katika mambo ya uhai wa dunia, lakini kuhusu Aakhirah wameghafilika [nayo].”[1]

Kilichowapelekea katika jambo hilo ni mapenzi yao makubwa kuyapenda maisha ya dunia na vyeo vyake. Lau wangeyapa kisogo maisha ya dunia, wakatamani maisha ya Aakhirah na wakazipendea nafsi zao wenyewe na waja wa Allaah kheri, basi wangelishikamana barabara na yale aliyoteremsha Allaah juu ya Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wakawahimiza watu mambo hayo. Hapo ndipo wengi wa watu wasingetoka nje ya uchaji Allaah na pia wakatosheka na yale yaliyomo ndani ya Qur-aan na Sunnah na wachache tu ndio wangetoka nje ya viwili hivyo, kwa sababu Allaah huwateua watu wenye kuyafahamu maandiko ya Qur-aan na Sunnah na kuwafanya wale waliotoka nje kuyarejelea. Wasingehitajia tena yale matawi yaliyozuliwa yanayotokana na mafumbo na njama zilizoharamishwa ambazo zimefungua njia za kuingia ndani ya ribaa na mambo mengine ya haramu ambayo yamehalalisha maharamisho ya Allaah kwa kutumia angalau kitimbi kidogo mno kama walivofanya watu wa Kitabu.

فَهَدَى اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا لِمَا اخْتَلَفُوا فِيهِ مِنَ الْحَقِّ بِإِذْنِهِ ۗ وَاللَّـهُ يَهْدِي مَن يَشَاءُ إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ

“Allaah akawaongoza wale walioamini kuiendea haki katika yale waliyokhitilafiana kwa idhini Yake na Allaah humwongoza amtakaye kuelekea njia iliyonyooka.”[2]

Swalah na amani zimwendee bwana wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake mpaka siku ya Qiyaamah. Allaah ni Mwenye kututosheleza Naye ndiye mbora wa kutegemewa.

[1] 30:7

[2] 02:213

  • Mhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn bin Rajab al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan Fadhwl ´Ilm-is-Salaf ´alaa ´Ilm-il-Khalaf, uk. 93-95
  • Imechapishwa: 04/10/2021