38. Mwenye kuwatii wanachuoni na viongozi katika kuharamisha aliyohalalisha au kuhalalisha aliyoharamisha Allaah amewafanya ni waungu badala ya Allaah

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Ibn ´Abbaas amesema:

“Kumekurubia kukushukieni mawe kutoka mbinguni; nawaambieni: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema na nyinyi mnanambia Abu Bakr na ´Umar wamesema.”[1]

2- Imaam Ahmad bin Hanbal amesema:

“Nashangazwa na watu ambao wanajua cheni ya wapokezi na usahihi wake wanaiacha na kufuata maoni ya Suftaan. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ

“Basi watahadhari wale wanaokhalifu amri yake; isije kuwapata fitina au ikawapata adhabu iumizayo.” (an-Nuur 24:63)

Unajua ni nini fitina? Fitina ni shirki. Pengine ataporudisha baadhi ya maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaingiwa moyoni mwake na kitu kama mashaka na upotevu na matokeo yake akaangamia.”

3- ´Adiy bin Haatiym amesimulia kwamba amemsikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisoma Aayah hii:

اتَّخَذُوا أَحْبَارَهُمْ وَرُهْبَانَهُمْ أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللَّـهِ

“Wamewafanya marabi wao na watawa wao kuwa ni waungu badala ya Allaah.” (at-Tawbah 09:31)

Nikamwambia: “Sisi hatukuwa tukiwaabudu.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Je, hawakuwa wakiharamisha aliyoyahalalisha Allaah nanyi mkayaharamisha na wakihalalisha aliyoyaharamisha Allaah nanyi mkayahalalisha?” Nikajibu: “Ndio.” Ndipo akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Huko ndio kuwaabudu.”[2]

Ameipokea Ahmad na at-Tirmidhiy ambaye ameifanya kuwa ni nzuri.

MAELEZO

Amechokusudia mwandishi kwa mlango huu ni kuhakikisha Tawhiyd na kutendewa kazi Shari´ah. Kadhalika kuadhimisha maamrisho na makatazo ya Allaah na vilevile kutahadhari kuwafuata kichwa mchunga wanachuoni na viongozi katika mambo yanayopingana na Shari´ah ya Allaah. Huku ni kufuata kwa kipofu.

Ni wajibu kwa wanachuoni na waumini kuadhimisha maamrisho na makatazo ya Allaah, wahalalishe aliyohalalisha Allaah na waharamishe aliyoharamisha Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wasimtii yeyote katika kwenda kinyume na hayo. Wengine wanatiiwa tu katika mema. Ni haramu kumtii yeyote katika jambo linalopingana na Shari´ah. Haifai kumtii kiumbe katika jambo la kumuasi Muumba. Haijuzu hata kwa mtu kuwatii wazazi wake, mtoto wake au mke wake katika jambo linalopingana na Shari´ah katika ya halali na ya haramu.

1- Ibn ´Abbaas amesema:

“Kumekurubia kukushukieni mawe kutoka mbinguni; nawaambieni: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema na nyinyi mnanambia Abu Bakr na ´Umar wamesema.”

Haya ni matishio ya adhabu. Anachotaka kusema ni kwamba anatumia hoja kwao kwa amri ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo mnakwenda kinyume na kurudisha amri ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa maneno ya Abu Bakr na ´Umar. Hii ina maana kwamba haijuzu kwenda kinyume na amri ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) japokuwa maoni yatakuwa ni yenye kutoka kwa Abu Bakr na ´Umar ambao ndio watu bora kabisa baada ya Mitume – mtu asemeje yakiwa ni maoni ya wengine? Hapa Ibn ´Abbaas anashaji´isha kufuata Shari´ah na kutahadharisha kuwaadhimisha watu katika mambo yanayopingana na Shari´ah.

2- Imaam Ahmad bin Hanbal amesema:

“Nashangazwa na watu ambao wanajua cheni ya wapokezi na usahihi wake wanaiacha na kufuata maoni ya Suftaan. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ

“Basi watahadhari wale wanaokhalifu amri yake; isije kuwapata fitina au ikawapata adhabu iumizayo.” (an-Nuur 24:63)

Unajua ni nini fitina? Fitina ni shirki. Pengine ataporudisha baadhi ya maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaingiwa moyoni mwake na kitu kama mashaka na upotevu na matokeo yake akaangamia.”

Bi maana wamejua cheni ya wapokezi kuwa ni sahihi kwenda kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah. Imaam Ahmad anamkaripia yule mwenye kufanya hivo na kwamba haimstahikii. Halafu akasoma:

فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ

“Basi watahadhari wale wanaokhalifu amri yake; isije kuwapata fitina au ikawapata adhabu iumizayo.”

Yule mwenye kurudisha kitu kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuna khatari kwake akapewa mtihani na akaingia katika shirki na kuritadi. Katika haya pia kuna maonyo ya kwenda kinyume na Shari´ah. Haijalishi kitu hata kama yule aliyefanya hivo ni mwanachuoni mkubwa. Maswahabah na wale waliokuja baada yao wamesema wazi kwamba haijuzu kuwatii katika jambo linalopingana na amri ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Matishio haya yanamuhusu yule mtu ambaye anajua kuwa maoni ya mtu fulani yanapingana na Shari´ah pamoja na hivyo akahalalisha kitu ambacho ni haramu.

3- ´Adiy bin Haatiym amesimulia kwamba amemsikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisoma Aayah hii:

اتَّخَذُوا أَحْبَارَهُمْ وَرُهْبَانَهُمْ أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللَّـهِ

“Wamewafanya marabi wao na watawa wao kuwa ni waungu badala ya Allaah.” (at-Tawbah 09:31)

Nikamwambia: “Sisi hatukuwa tukiwaabudu.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Je, hawakuwa wakiharamisha aliyoyahalalisha Allaah nanyi mkayaharamisha na wakihalalisha aliyoyaharamisha Allaah nanyi mkayahalalisha?” Nikajibu: “Ndio.” Ndipo akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Huko ndio kuwaabudu.”

Ameipokea Ahmad na at-Tirmidhiy ambaye ameifanya kuwa ni nzuri.

Hii ina maana kwamba yule mwenye kuwatii wanachuoni na viongozi katika kuharamisha kitu cha halali au kuhalalisha kitu cha haramu na wakati huohuo akaonelea kuwa kufanya hivo kunafaa na yeye anajua kuwa kunaenda kinyume na Shari´ah ya Allaah, huku ni kuwaabudu na amekufuru. Ama ikiwa anawafuata kwa sababu ya ujinga na Ijtihaad, sio kuwaabudu na wala haingii katika matishio. Kwa sababu mtu anatakiwa kuwauliza wanachuoni na kuchukua fatwa zao maadamu hajui kuwa jambo hilo linapingana na Shari´ah ya Allaah.

[1] Ahmad (3121).

[2] at-Tirmidhiy (3095), at-Twabaraaniy katika ”al-Mu´jam al-Kabiyr” (218), al-Bayhaqiy katika ”as-Sunan al-Kubraa” (20137). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Ghaayat-ul-Maraam” (6).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 122-123
  • Imechapishwa: 27/10/2018